MAHAKAMA KUU YATUPILIA MBALI KESI YA SPIKA NDUGAI NA CECIL MWAMBE


Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetupilia mbali kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na wakili Paul Kaunda dhidi ya Spika wa Bunge, Job Ndugai akiomba mahakama hiyo kutengua amri ya Spika kumtambua Cecil Mwambe kama mbunge halali wa Ndada ikisema amekosea kufungua shauri hilo.



Mbali na Ndugai, walalamikiwa wengine ni Mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Katika kesi hiyo Wakili Kaunda anaiomba Mahakama Kuu kutengua amri ya Spika Ndugai ya kumtambua  Mwambe kama Mbunge halali wa Ndanda.

Katika uamuzi mdogo uliosomwa leo Juni 3, 2020 na Jaji Issa Maige aliyekuwa akisaidiana na Jaji Stephen Magoiga na Jaji Seif Kulita amesema mlalamikaji alikosea namna ya kufungua kesi ya kikatiba badala yake alipaswa kufungua kesi kwa utaratibu wa kawaida.

Amesema,  kauli ya Spika Ndugai aliyoitoa haikuwa imevunja katiba bali ni ya kiutaratibu katika shughuli zake za kiutendaji hivyo mlalamikaji angekuwa sahihi kama angefungua kesi hiyo kwa utaratibu wa kawaida kwa kutumia Ibara ya 83 (1) badala ya ile ya 26 (2) aliyoitumia.

Jaji Maige amesema Ibara hiyo inaenda sambamba na kifungu cha 37 cha Sheria ya Uchaguzi ambacho kinaeleza kuhusu utaratibu wa kutangaza kiti cha Mbunge ambacho kiko wazi.

Wakili Kaunda alifungua  kesi mahakamani hapo dhidi ya  Ndugai, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Ndanda kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)  Cecil  Mwambe  na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Katika kesi hiyo Wakili Kaunda anadai Mwambe alitangaza kujivua uanachama wa Chadema na kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM) kauli ambayo iliungwa mkono na katibu mkuu wa CCM Dk  Bashiru Ally  aliyempokea rasmi  Mwambe mbele ya hadhira kwa kumkabidhi kadi ya CCM, na  Mwambe naye alimkabidhi Katibu Mkuu huyo  kadi yake ya Chadema.

Wakili Kaunda anadai  kitendo cha Spika kumtambua  Mwambe kama mbunge halali wakati  ameshajivua uanachama wa chama kilichomdhamini kama Mbunge wa  Ndanda (2015-2020), ni ukiukwaji wa ibara ya 71(1)(f) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 na hakuna mamlaka yoyote nchini, achilia mbali Spika, yenye uwezo wa ku mrudisha bungeni Mbunge ambaye kwa hiari yake mwenyewe ameamua kujivua uanachama wa chama cha siasa kilichomdhamini kupata ubunge.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post