Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAKAMU WA RAIS KUONGOZA UJUMBE WA TANZANIA KATIKA SHEREHE ZA KUAPISHWA KWA RAIS MTEULE WA BURUNDI


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuongoza ujumbe wa Tanzania kwenda Nchini Burundi kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais Mteule wa Burundi Mhe Evariste Ndayishimiye hapo kesho June 18,2020.

Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi ameyasema hayo Jijini dar es Salaam katika Ubalozi wa Burundi Nchini Tanzania alipokwenda Ubalozini hapo kwa ajili ya kusaini kitabu cha maombolezo kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Burundi Mhe. Pierre Nkurunziza aliyefariki June 09,2020 kwa maradhi ya Moyo.

Ameongeza kuwa kutokana na mahusiano ya karibu yaliyopo baina ya Burundi na Tanzania Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameamua kuongeza ujumbe wa Tanzania kwenda Burundi ambapo mbali na kuongozwa na Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan pia ataambatana na Rais Mstaafu wa awamu ya nne Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete.

Prof. Kabudi amesema kuwa Hayati Pierre Nkurunziza amefanya kazi kubwa sana ya kuiunganisha Burundi na kuifanya nchi hiyo kuwa moja ya nchi zenye umoja na amani katika bara la Afrika lakini pia kuirejeshea Burundi matumaini na amani ya demokrasia na kudhihirika katika uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka huu na kumalizika kwa amani.

Kwa upande wake Balozi wa Burundi Nchini Tanzania Balozi Gervais Abayeho amesema Ubalozi huo na Warundi kwa ujumla wamepokea kwa mshtuko na majozi taarifa za kifo cha Rais Pierre Nkurunziza hasa ukichukulia kuwa baada ya kumalizika kwa uchaguzi Rais huyo alikuwa akiendelea na shughuli zake kama kawaida ikiwa ni pamoja na kufanya mazoezi.

Ameongeza kuwa wakati wakiendelea na maombolezo ya kiongozi huyo wa Burundi,Warundi wote wanamshukuru Mungu kwa tayari alikwishapatikana kiongozi mwingine ambaye ni Rais Mteule Evariste Ndayishimiye na mara baada ya kuapishwa kwake kuwa Rais mpya wa Burundi ndipo shughuli nyingine ikiwa ni pamoja na kufahamu siku ya kufanyika kwa maziko ya Rais Pierre Nkurunziza.

Rais Pierre Nkurunziza alifariki dunia June 09,2020 kutokana na ugonjwa wa moyo alipokuwa akipatiwa matibabu katika hospitali ya Natwe Turashoboye iliyopo mkoani Karuzi,mashariki mwa Burundi.

Bwana ametoa Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com