Picha hauhusiani na habari hapa chini
Na Mwandishi wa Malunde 1 blog
Wafanyakazi wanne wa kiwanda cha uchenjuaji wa madini ya dhahabu(Plant) katika Mgodi mdogo wa Ntambalale, kijiji cha Wisolele Kata Segese Halmashauri ya Msalala Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga,wameuawa na mmoja kujeruhiwa kwa kucharangwa na mapanga na watu wasiojulikana kisha kutokomea na kaboni zaidi ya kilo 200.
Waliofariki dunia wanatajwa kuwa ni Daniel (Operator), Raphael Heman Kipeya (msimamizi wa Plant), Lusajo Marco Mwanasangula (mlinzi), Juma Jiswanya (mlinzi ambapo walikuwa wafanya kazi katika Rush namba 4 inayomilikiwa na Dadi Marco.
Mwenyekiti wa mgodi wa Ntambalale Hamisi Mabubu amesema tukio hilo limetokea majira ya saa tisa usiku wa kuamkia leo Jumanne Juni 30, 2020 katika moja ya viwanda vya uchenjuaji wa madini.
“Wafanyakazi watano wa kiwanda hicho, walivamiwa na kucharangwa na mapanga sehemu mbalimbali za miili yao na watu wasiojukulikana na kuwapora kaboni, Wafanyakazi wanne walipoteza maisha papo hapo na mmoja aliyejulikana kwa jina la Evary Mbuya akijeruhiwa. Bila shaka chanzo cha tukio hili ni tamaa ya kupata mali kwa haraka”, amesema.
Naye Diwani wa Kata ya Segese Joseph Mayala amesema alipata taarifa ya tukio hilo kutoka kwa mtendaji wake wa kata majira ya saa kumi usiku na walipofika kwenye tukio walikuta miili ya watu wanne na mmoja wao Evary Mbuya walimkimbiza katika Hospitali ya Halmashauri ya mji wa Kahama kwa ajili ya matibabu.
Hata hivyo Mayala amesema matukio ya uvamizi wa viwanda cha uchenjuaji wa dhahabu yamekuwa yakitokea mara kwa mara hasa wakati wamiliki wa viwanda wakiwa na kaboni,na kuliomba jeshi la polisi kuongeza ulinzi na kudhibiti majanga haya yasiendelee kutokea.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Joseph Paul,amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa harakati za kuwatafuta na kuwatia nguvuni walitotenda tukio hilo zinaendelea na wakibainika watafikishwa katika vyombo vya sheria.
Social Plugin