Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Chisegu, Halmashauri ya Mji wa Masasi, mkoani Mtwara, Mohamedi Mboloma, amekutwa amejinyonga msituni baada ya kutoweka nyumbani kwake kwa siku tatu bila kuaga.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo wakati akiongea na Nipashe jana, ofisa wa Jeshi la Polisi ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa kuwa sio msemaji, alisema tukio hilo limegundulika jana katika msitu huo uliopo nje kidogo ya kijiji cha Mbaju, Kata ya Chigugu huku mwili ukiwa juu ya mti ukining’inia.
Alisema mwalimu huyo ambaye ni mwenyeji wa Mtwara mjini, anadaiwa kabla ya kufanya uamuzi huo alitoweka nyumbani kwake kwa siku tatu bila ya kuaga wala kutoa taarifa kwa familia yake.
Alisema inadaiwa kuwa alitoweka nyumbani tangu Juni 16, saa 10 jioni akiwa na gari lake dogo na kuelekea katika matembezi yake kama kawaida na hakuonekana tena hadi mwili wake ulipokutwa ukining’nia msituni.
Alisema mwalimu huyo amekutwa akiwa amejinyonga kwa kutumia mkanda wake wa suruali pamoja na kamba na kwamba alikwenda katika msitu huo na kuliacha gari lake kando na kujinyonga.
“Marehemu alifika huku akiwa na gari lake na inaonekana baada ya kufika hapa aliweka simu zake zote mbili ndani ya gari na kufunga milango ya gari kisha kuingia msituni na kutimiza azma yake hiyo ya kujinyonga,” alisema.
Alisema Jeshi la Polisi baada ya kupata taarifa ya kupotea kwa mwalimu huyo na baadaye kuonekana gari lake likiwa karibu na msitu huo, lilifanya msako katika msitu huo.
Alisema msako huo ulifanyika jana kwa kushirikiana na wanakijiji wa kijiji hicho kwa kuingia ndani ya msitu huo kutamfuta, lakini hata hivyo hawakuweza kumpata.
Alisema, jana wananchi waliingia tena msituni, lakini upande wa pili ndipo walipokuta mwili huo wa marehemu ukiwa juu ya mti ukining’inia.
Alisema jeshi hilo linachunguza chanzo cha mwalimu huyo kujinyonga na upelelezi unaendelea.
Alisema polisi wameshautoa mwili kwa ajili ya kuwakabidhi ndugu zake ili waendelee na taratibu zingine za mazishi.
Social Plugin