Msaidizi mkuu wa Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela na kazi ngumu kutokana na hatia ya ufisadi.
Vital Kamerhe, mwenye umri wa miaka 61 na aliyehudumu kama mkuu wa utumishi kwenye Ikulu ya Kinshasa, alitiwa hatiani kwa ufisadi wa zaidi ya dola milioni 50, kwa mujibu wa mahakama kuu mjini Kinshasa.
Sehemu kubwa ya fedha hizo zilikuwa zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba 1,500, chini ya programu iliyotangazwa na Tshisekedi mara tu baada ya kuapishwa Januari 2019.
Hii ni mara ya kwanza kwa wale wanaochukuliwa kama vigogo wasiogusika nchini Kongo kushitakiwa na kuhukumiwa kwa ufisadi.
Kamerhe, ambaye anatambulika kama mwanasiasa mjanja anayecheza karata zake takribani katika kila utawala, alikuwa pia mshirika mkuu wa rais wa zamani, Joseph Kabila, kabla hajaungana na kambi ya Tshisekedi.
Social Plugin