Baada ya CHADEMA kuwataka watangaza nia ya kugombea nafasi ya Urais ndani ya chama hicho wajitokeze, NCCR Mageuzi nao wamesema kuwa wanatarajia kutoa ratiba ya uteuzi wa wagombea Urais, Ubunge na Madiwani wiki ijayo, na kuiomba Tume ya Taifa ya Uchaguzi kutenda haki katika uchaguzi ujao.
Pia, chama hicho kimefungua milango kwa chama chochote cha siasa nchini, ambacho kipo tayari kushirikiana ili kuiondoa Serikali ya Chama cha Mapinduzi madarakani.
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alibainisha hayo jana wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dodoma.
Mbatia alisema, tayari ameshamwagiza Katibu Mkuu wa chama hicho kutoa ratiba ya uteuzi wa wagombea ndani ya chama mapema wiki ijayo.
“Nitoe wito kwa vijana na wale wote wenye sifa, kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali, katika uchaguzi huu, nafasi za urais Tanzania bara na Zanzibar, ubunge, wawakilishi pamoja na zile za udiwani,” alifafanua Mbatia.
Alisema, katika uchaguzi mkuu mwaka huu, chama hicho kipo tayari kushirikiana na vyama vingine vya siasa kwa maslahi ya taifa.
“Sisi tupo tayari kushirikiana na chama chochote kile cha siasa kwa maslahi ya mama Tanzania, kwani hata salamu yetu inasema kwa pamoja tutashinda,” alisema Mbatia.
Social Plugin