Nchi za NORDIC ambazo ni Norway, Sweden, Finland na Dernmark zimeahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania na kuhakikisha kuwa Tanzania inasonga mbele katika maendeleo yake kijamii, kisiasa na kiuchumi.
Akiongea wakati wa maadhimisho ya wiki ya Nordic jijini Dar es Salaam, Balozi wa Norway nchini, Mhe. Elisabeth Jacobsen amesema kuwa nchi za Nordic zimeadhimisha wiki ya Nordic nchini Tanzania na zimejadili masuala ya malengo ya maendeleo endelevu ambapo pamoja na mambo mengine, wametumia wiki ya Nordic kuendeleza uhusiano na ushirikiano mkubwa uliopo kati ya Nordic na Tanzania.
"Wiki ya Nordic inatoa fursa ya kushirikiana na kujifunza mambo mbalimbali yakiwemo ya kijamii, kisiasa na kichumi pamoja na kupata uzoefu wa maendeleo kutoka kwa kila mmoja wetu," Amesema Balozi Jacobsen.
Ameongeza kuwa, nchi za Nordic zimejidhatiti kufanya kazi kwa karibu na Tanzania ili kuhakikisha kuwa Tanzania inasonga mbele katika maendeleo.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) akiongea mara baada ya kukabidiwa mpira ulioandikwa malengo 17 ya maendeleo endelevu ikiwa ni ishara ya kuhamasisha maendeleo ya Tanzania, Balozi wa Norway nchini amesema kuwa mpira huo ni ishara ya ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na nchi za Nordic.
"Ushirikiano wetu (Tanzania) na nchi za Nordic ni wa muda mrefu kabla ya uhuru na hata baada ya uhuru. Tumekuwa tukifurahia ushirikiano wetu na nchi za Nordic na umekuwa ukimarika kila wakati, ni matumaini yetu sisi kama serikali kuwa uhusiano utaendelea kuimarika zaidi," amesema Dkt. Ndumbaro
Mwezi Novemba 2019, ulifanyika Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya nje wa Afrika na Nordic, ambapo pamoja na mambo mengine, mkutano huo uzikutanisha nchi za Afrika na Nordic na kutoa fursa ya kujadili masuala mbalimbali yakiwemo, elimu, kilimo biashara na uwekezaji.