Rais Magufuli amesema Serikali yake itaendelea kushirikiana na walimu kuhakikisha sekta ya elimu inasonga mbele na kwamba madai yao anaendelea kuyashughulikia na kuyatatua moja baada ya jingine, hivyo hawezi kuwatupa kwani hata yeye alikuwa mwalimu kabla ya kuingia kwenye siasa.
Magufuli amesema hayo leo Ijumaa, Juni 5, 2020, wakati akihutubia kwenye mkutano mkuu wa chama cha walimu Tanzania (CWT), jijini Dodoma.
==>>Haya ni baadhi ya maneno aliyoyasema
“Ninamshukuru Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu, ametaja mambo ambayo tumeyafanya kwa miaka mitano iliyopita, moja ya mambo makubwa tuliyoyafanya kwenye elimu ni kutoa elimu bila malipo kuanzia shule za msingi hadi sekondari.
“Ndugu wajumbe wa mkutano huu, ninafahamu mkutano huu ni muhimu kwa ajili kuwapata viongozi wa walimu, nisingependa kuonekana nampigia chapuo mtu yeyote lakini uongozi huu unaomaliza muda wake umejenga uhusiano mzuri kati ya walimu na Serikali.
“Siwezi kuwatupa walimu, tunajenga nyumba moja, mimi nilikuwa mwalimu, kuwakana walimu ni kuikana nafsi yangu siwezi kuwatupa, naamini hata kama uongozi huu hautochaguliwa, huo uongozi ujao pia utajenga uhusiano mzuri na Serikali.
”Niwahakikishie walimu kuwa serikali hii imejaa walimu, hata mimi nikisahau nakumbushwa na Mama Janeth naye ni mwalimu, hata Majaliwa akisahau anakumbushwa na Mary Majaliwa tena mahala pazuri pa kukumbushwa, Waziri wa Madini ni mwalimu, hata Waitara ni mwalimu.
“Nilipotangaza kufunga vyuo na shule kupisha corona, kesho yake nikapigiwa simu na Rais wa CWT, akaniambia usifanye kama nchi nyingine ukakata mishahara ya walimu, nikatafakari, nikasema corona hata ikikaa miaka kumi sitakosa mshahara wa kuwalipa walimu.
“Napenda niwahakikishie walimu wote nchini, kuwa hata kama shule zingefungwa mwaka mzima au hata miaka kumi, tutaendelea kuwalipa mishahara yenu kama kawaida,kwa sababu Corona haikuletwa na walimu.
”Ili kuepuka udanganyifu, Serikali kwa sasa inaandaa mfumo wa kielektroniki wa kuhakiki madai ya watumishi wakiwemo walimu, ambao utaanza kutumiwa kwa majaribio mwezi huu hapa Dodoma na endapo utaonesha mafanikio utatumika kwa nchi nzima.”
“Kuhusu malimbikizo ya madeni, tangu Novemba 2015 Serikali imelipa shilingi bilioni 115, tutaendelea kulipa madeni hayo kadiri tutakavyokuwa tunayahakiki.
“Tumesogeza bajeti ya bodi ya mikopo ya elimu ya juu ya kutoka Sh.341 bilioni, mwaka 2014/2015, hadi kufikia Sh.450 bilioni,mwaka 2019/2020. Ufaulu wa kidato cha nne umeongezeka kutoka asilimi 69.8 mwaka 2015 hadi 89 mwaka 2019.
“Ualimu ndio sekta mama, na tunawathamini sana, hata kama corona itakaa miaka mitano tutawalipa mishahara yenu kama kawaida kwa kuwa walimu wao hawajaileta hiyo corona.
“Kwenye huu uchaguzi chagueni viongozi wenye uchungu na walimu, epukeni kuchaguana kwa kujuana au kwa rushwa, mtakaochaguliwa muwatumikie walimu sio kwa maslahi yenu binafsi” amesema.