Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RAIS MAGUFULI AZUNGUMZA NA WAZIRI MKUU WA INDIA NARENDRA MODI

Rais  wa Tanzania, John Pombe Magufuli amefanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi. 


Taarifa iliyotolewa na Gerson Msigwa, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, imesema, Modi amempigia simu Rais Magufuli leo Ijumaa tarehe 12 Juni 2020 na kuzungumzia masuala yahusuyo uhusiano na ushirikiano mzuri, wa kirafiki na kihistoria uliopo kati ya Tanzania na India.

Katika mazungumzo hayo, Modi amempongeza Rais Magufuli kwa uongozi wake wa awamu ya tano na amemtakia heri yeye na Watanzania wote katika juhudi kubwa za kuijenga nchi zinazoendelea na uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka 2020.

Pamoja na kumhakikishia India itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano wake na Tanzania katika nyanja mbalimbali hasa kiuchumi, Modi amempa mrejesho wa yaliyojiri katika mkutano wa nchi 20 tajiri duniani (G20) uliofanyika hivi karibuni (India ikiwa ni mojawapo).

Nchi hizo zimekubaliana taasisi za fedha za kimataifa zitoe msamaha wa madeni kwa nchi masikini na zinazoendelea, zilizopata madhara kutokana ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (Covid-19).

Rais Magufuli amemshukuru Modi kwa kumpigia simu, kumtakia heri na kumpa mrejesho wa yaliyojiri katika mkutano wa G20 na ameomba taasisi za fedha za kimataifa zitakapotoa msamaha wa madeni ziitupie macho Tanzania ambayo pia imepatwa na madhara ya ugonjwa wa Corona ili iweze kuimarisha uchumi wake.

Aidha, Rais Magufuli ameipongeza India kwa juhudi za kutafuta chanjo ya virusi ya Corona ambazo anaamini zitafanikiwa na kwamba Tanzania ikiwa moja ya nchi zilizokubwa na ugonjwa huo itanufaika, japo ugonjwa wenyewe unapungua kwa kasi kubwa hapa nchini.

Rais Magufuli amemshukuru Modi kwa uhusiano na ushirikiano mzuri wa Tanzania na India ambayo ni miongoni mwa nchi tano zinazoongoza kwa uwekezaji hapa nchini na pia ameshukuru kwa mikopo nafuu inayotolewa na India kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa Tanzania.

Ameitaja baadhi yake ni mkopo wa ujenzi wa Taasisi ya Teknolojia ya Nelson Mandela, mikopo ya miradi ya maji na ufadhili wa masomo ya elimu ya juu kwa wanafunzi wa Tanzania wanaokwenda kusomea masuala ya afya, uhandisi na Tehama nchini India.

Mikopo ya miradi ya maji ni pamoja na Sh. 225.9 bilioni  (Ruvu- Dar es Salaam, ambao umekamilika), Sh. 611.5 bilioni  (Maji ya Ziwa Victoria kwenda Tabora, Nzega na Igunga ambao unakaribia kukamilika), Sh. 1. 2 Trilioni (miradi ya maji ya Miji 28, ambayo utekelezaji wake unaendelea) na Sh. 209.9 bilioni  (miundombinu ya maji ya Zanzibar, ambayo inaendelea kujengwa).

Rais Magufuli amemhakikishia Waziri Mkuu, Modi kuwa Tanzania itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wake na India, na amewaalika wafanyabiashara na wawekezaji wa India kuja kuwekeza hapa nchini katika sekta mbalimbali zikiwemo viwanda, kilimo, ufugaji, madini na nyingine kwani Tanzania imejenga mazingira mazuri ya uwekezaji.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com