Rais Magufuli amewataka Watanzania kutotilia maanani baadhi ya maneno ya uongo kutoka kwa watu wa nje, kuhusu milipuko ya magonjwa mbalimbali huku akisimulia namna alivyomfuta kazi kiongozi mmoja wa taasisi ya umma baada ya kutangaza taarifa za uongo kuhusu uwepo wa ugonjwa wa Zika nchini Tanzania.
Akizungumza leo Ijumaa, Juni 5, 2020, katika Mkutano Mkuu wa Chama Cha Walimu Tanzania unaofanyika katika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma, Rais Magufuli amesema Watanzania wasitishwe wala wasiwe na hofu kuhusu Ugonjwa wa Corona kwani unaelekea kuisha kabisa.
“Wakati tunaingia madarakani tuliambiwa Tanzania kuna ugonjwa unaitwa Zika, aliyetangaza na aliyetumiwa kutangaza nikamfukuza kazi, bahati mbaya ni Mgogo
“Baada ya kumfukuza yule Mgogo aliyesema Tanzania kuna Zika na waliomtuma wakamteua kuwa Mkurugenzi, mpaka leo miaka karibu mitano hapajawahi kuwa na kesi ya Zika hapa Tanzania.
“Baada ya uzushi wa Zika kupita na nilipomfukuza kazi aliyesema kuna Zika,tukakaa baadaye tukaambiwa kuna Ebola, walijua wakisema tuna Ebola watalii hawatokuja, tukasema sisi hatuna Ebola, wala mjukuu au hawara yake Ebola, na kweli hatujaona mgonjwa amekufa kwa Ebola Tanzania.
“Umekuja ugonjwa wa Corona walikuwa wanazungumza kwamba maiti zitazagaa kwenye barabara hasa Afrika, wao walikuwa watabiri walishindwa kuelewa Mungu analipenda taifa la Tanzania pamoja na Afrika,” amesema