Serikali imekiagiza Chuo cha Diplomasia kujikita kuongeza tafiti pamoja na machapisho mbalimbali kwa lengo la kuwawezesha wahitimu wa chuo hicho kutoa mchango wao katika Taifa hususani wakati huu wa utekelezaji wa sera ya Diplomasia ya Uchumi.
Maagizo hayo yametolewa leo jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) wakati alipotembelea chuo hicho na kuongea na wahadhiri, wafanyakazi pamoja na wanafunzi.
Dkt. Ndumbaro amesema ili chuo cha diplomasia kiendelee kuheshimika zaidi duniani lazima kihakikishe kuwa kinazalisha tafiti na machapisho ya kutosha.
"Utafiti na machapisho siyo suala la wahadhiri peke yao…..siyo suala la wanafunzi peke yao ni suala la wanachuo…… mawazo yenu lazima yafanyiwe utafiti kwa kushirikiana na wahadiri wenu na ni lazima tuwe na machapisho zaidi," Amesema DKt. Ndumbaro
Naibu Waziri ameongeza kuwa moja kati ya changamoto inayoikumba diplomasia hivi sasa ni mabadiliko ya mifumo mbalimbali duniani ambapo wanadiplomasia wanapaswa kujua kuwa dunia ipo katika mlengo upi, hivyo vyema mkajikita katika tafiti zenu ili kuweza kusaidia kufafanua masuala ya kidiplomasia na uhusiano wa kimataifa yanayotokea duniani.
"Lakini pia niliagiza muongeze lugha zaidi kwa sababu pia diplomasia pia ni mawasiliano na unawasiliana na watu wa lugha tofauti tofauti, kwa hiyo tuongeze lugha mbalimbali ili diplomasia iweze kufanya kazi yake," Amesema DKt. Ndumbaro.
Aida, Naibu Waziri ameagiza pia chuo hicho kuanzisha semina za kila mwezi ambapo zitajumuisha Wahadiri na wanafunzi pamoja na mabalozi wastaafu kwa lengo la kujadili mambo yanayohusu diplomasia na kuwapa uzoefu wa masuala ya kidiplomasia.
Wanafunzi kwa upande wao wamepata fursa ya kumuelezea Naibu Waziri changamoto mbalimbali zinazo wakabili zikiwemo za kupata asilimia ndogo za mkopo wa elimu ya juu, ukosefu wa mafunzo kwa vitendo, ukosefu wa mabweni pamoja na mazingira ambayo siyo wezeshi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.
"Mkopo tunaopewa ni mdogo sana na hautoshi hivyo tunaomba serikali itusaidie kutuongezea fedha za mkopo ili tuweze kukidhi mahitaji yetu wakati tunapokuwa chuoni,"Amesema Isack Sadock
Pia, Dkt. Ndumbaro baada ya kusikiliza changamoto zinazowakabili wanafunzi chuoni hapo, ameuagiza uongozi wa chuo kuandaa na kuratibu mafunzo kwa vitendo badala ya kufuatiliwa na wanafunzi, kutoa huduma stahiki kwa wanafunzi wenye ulemavu/maitaji maalumu ili waweze kusoma katika mazingira mazuri.
Nae Kaimu Mkuu wa Chuo cha Diplomasia, Dkt. Jeremia Ponera amemhakikishia Naibu Waziri kuwa chuo kitayafanyia kazi na kuyatekeleza maagizo yote aliyoyatoa.
"Mhe. Naibu Waziri naomba nikuhakikishie kuwa maagizo yako tumeyapokea……….mimi kwa kushirikiana na menejimenti, wahadhiri na wafanyakazi tayafanyia kazi kwa wakati," Amesema Dkt. Ponera
Aidha, Naibu Waziri, Dkt. Ndumbaro amekagua mradi wa ujenzi wa jengo jipya la chuo cha Diplomasia.
Katika hatua nyingine, ametoa msimamo wa Serikali kuhusu changamoto zinazojitokeza mipakani hasa katika mpaka wa Tanzania na Kenya na kusema kuwa Serikali ipo kwenye mazungumzo na Kenya ili kuweza kubaini tatizo ni kitu gani.
"Kwa sasa tupo kwenye majadiliano na wenzetu wa Kenya na kuona tatizo ni kitu gani je ni corona tu au ni zaidi ya corona? Msimamo wa serikali yetu ni kuwa kila nchi ipime watu wake…..na tunaamini huo ndiyo msimamo sahihi wa diplomasia ya uchumi," Amesema Dkt. Ndumbaro.
Chuo cha Diplomasia kilianzishwa rasmi tarehe 13 Januari 1978 kwa kusainiwa Makubaliano yaliyofanywa na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wa wakati huo, Mhe. Benjamini William Mkapa wa Tanzania na Mhe. Joaquim Chissano wa Msumbiji.
Social Plugin