Kushoto ni Bibi Susana Mmari wakati wa uhai wake, kulia ni mazishi yake.
Hivi karibuni kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii, zilisambaa video na picha zikionesha watu wakisherehekea kifo cha Bibi mmoja aliyejulikana kwa jina la Susana Benjamin Mmari, aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 131, kilichotokea Mei 27 na kuzikwa Mei 30, 2020, huko Old Moshi Kidia.
Mmoja wa wajukuu wa Bibi huyo, anayejulikana kwa jina la Noel Mmari amesema kuwa waliamua kuugeuza msiba huo kama sherehe, kwa sababu ilikuwa ni shukrani kwa Mungu kutokana na Neema kubwa aliyowapa kupitia maisha ya Bibi yao.
"Bibi alikuwa na watoto sita, wa kiume 4 na wanawake walikuwa 2, na wawili tayari walishafariki, kaacha wajukuu 97, vitukuu 370, hivyo jumla ameacha uzao wa watu 586, tulimzika kwa shangwe kwa sababu afya yake mwishoni ilikuwa kama anateseka, kwa hiyo kitendo cha kutwaliwa tukaona tukisikitika tutamkosea Mungu, sababu katupa Neema ambayo tunatakiwa kumshukuru siyo kusikitika" amesema Noel.
Aidha Noel amesimulia Bibi Suzana alikuwa ni wa aina gani, "Bibi alikuwa akiamka asubuhi anaenda shamba na alichokuwa anakilima ndiyo hicho hicho alikuwa anakula na wanaye na wajukuu na mimi alinilea baada ya kumaliza chuo na kupata kazi, ilibidi nimchukue niishi naye, kwahiyo amefariki akiwa kwenye mikono yangu, mimi ni miongozi mwa wajukuu zake wadogo, nina miaka 40 sasa".
Chanzo- EATV
Social Plugin