Simba SC wamezidi kujisogeza jirani na taji la tatu mfululizo la ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya wenyeji, Mbeya City jioni ya leo Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya.
Shujaa wa Simba SC leo alikuwa ni Nahodha wake, mshambuliaji John Raphael Bocco aliyefunga mabao yote hayo mawili, moja kila kipindi.
Kwa ushindi huo, Simba SC inafikisha pointi 78, sasa ikiizidi pointi 20 Azam FC inayofuatia katika nafasi ya pili baada ya wote kucheza mechi 31.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Athumani Lazi wa Morogoro, aliyesaidiwa na Abdallah Rashid wa Pwani na Abdulaziz Ally wa Arusha, Bocco alifunga bao la kwanza dakika ya tano akimalizia pasi ya kiungo Mzambia, Clatous Chota Chama na la pili dakika ya 54 akimalizia pasi ya kiungo Mkenya, Francis Kahata Nyambura.
Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Kagera Sugar imeibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Azam FC Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, bao pekee la Yusuph Mhilu dakika ya 33.
Biashara United imeichapa KMC FC 4-0, mshambuliaji Atupele Green Jackson akipiga hat trck kwa mabao yake ya dakika za 68, 72 na 90 na ushei, baada ya Justine Omary kufunga la kwanza dakika ya 36.
Bao la dakika ya 80 la kiungo Pius Buswita likainusuru Polisi Tanzania kulala mbele ya Alliance FC iliyotangulia kwa bao la Martine Kiggi dakika ya 51 timu hizo zikitoka sare 1-1 Uwanja wa Nyamagana Jijini Mwanza.
Mchezo mwingine wa Ligi Kuu unafuatia Saa 1:00 usiku Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam baina ya Yanga SC na Namungo ya Ruangwa mkoani Lindi.
Kikosi cha Mbeya City leo kilikuwa; Aaron Kalambo, Keneth Kunambi/ Suleiman Mangoma dk90, Mpoki Mwakinyuke, Roland Msonjo, Ibrahim Ndunguli, Emmanuel Memba, Suleiman Ibrahim, Abdul Suleiman, Abasarim Chidiebele, Peter Mapunda na George Chota.
Simba SC; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Kennedy Juma, Pascal Wawa, Gerson Fraga ‘Viera’, Said Ndemla/Muzamil Yassin dk73, Clatous Chama, John Bocco, Miraj Athumani ‘Madenge’na Francis Kahata/Luis Miquissone dk55.
Chanzo - Binzubeiry blog