Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KAMPENI SITETEREKI TULONGE AFYA YASHIKA KASI


Mmoja wa wanamuziki nyota nchini kwa jina la kisanii aitwaye Lady Jay Dee akitumbuiza kwenye moja ya tamasha hilo hivi karibuni jijini Dar es salaam.

****
Kampeni ya SITETEREKI Tulonge Afya ambayo ilizinduliwa hivi karibuni ikiwa ni mahususi kwa ajili ya vijana wa Kitanzania imeendelea kushika kasi. SITETEREKI ni jukwaa maalum la mawasiliano ya kubadilisha tabia linalowalenga vijana huku lengo ikiwa ni kuwa kimbilio kwa vijana, kuwa sehemu ambayo vijana wataungana, wakiiamini na kuitegemea, inayowapa hamasa na taarifa zitakazowawezesha kujiboresha, na kuboresha maisha yao. 

SITETEREKI itasaidia kuunganisha na kuboresha shughuli za mawasiliano ya mabadiliko ya tabia kwa vijana nchiniTanzania ili kuwahamasisha kuwa na tabia za kiafya ambazo zitaboresha hali zao na afya zao kwa ujumla.

Akizungumza jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi Mkazi wa shirika la USAID Tanzania Andy Karas alisema kuwa SITETEREKI ni mahususi kwa ajili ya vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24. Hata hivyo jukwaa hili litatoa taarifa za kiafya ambazo zitawanufaisha vijana wote na kuhamasisha tabia ambazo zitakuwa zinamlenga kila kijana wa Kitanzania bila kujali umri wake, jinsia au hali yake ya kiuchumi.

Karas aliongeza, ‘SITETEREKI imeundwa kuwapatia vijana taarifa sahihi, kuwapa hamasa na kuwajengea ujuzi unaokidhi mahitaji yao ya sasa. Jukwaa hili litawafikishia vijana taarifa za afya kupitia vyanzo mbalimbali vya mawasiliano, kwa kutumia vyombo vya habari kama vile redio, mbinu mbali mbali za kijamii, mawasiliano ya ana kwa ana, pamoja na mbinu za kidijitali na mitandao ya kijamii, ili kuwahamasisha kuwa na tabia za kiafya na kujijengea maisha chanya.’

Alisema kuwa Jukwaa la SITETEREKI lipo chini ya uangalizi wa Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, likiwezeshwa na Watu wa Marekani kupitia Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Watu wa Marekani (USAID) ndani ya mradi wa miaka mitano wa USAID Tulonge Afya (2017 – 2022) unaotekelezwa na FHI360. 

‘SITETEREKI inalenga maeneo yatakayoonesha mafanikio makubwa katika kuboresha maisha, afya na ustawi wa vijana wa Kitanzania wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24 kwa kuwa takwimu zinaonyesha kuwa maambukizi ya VVU na mimba zisizotarajiwa huchangia kwa kiasi kikubwa vijana kuwa na afya duni, na vifo vya vijana. Hata hivyo, wigo wa jukwaa hili unaweza kutanuka ili kufikia maeneo mengine ya kiafya na makundi mengine ya vijana,’ Karas aliongeza.

Mkurugenzi wa Miradi Tulonge Afya Waziri Nyoni alisema kuwa SITETEREKI inawezesha ufikiwaji wa malengo makuu ya kudhibiti maambukizi ya UKIMWI kwa vijana na katika afya ya uzazi, kwa kuhamasisha tabia kwa vijana wasiooa/olewa wenye kati ya miaka kama matumizi za afya ya uzazi, matumizi ya kondomu kwa usahihi na kila mara, kupima VVU na kuanza matumizi ya ARV mapema kama una maambukizi, kuzingatia matibu kama unaishi na VVU na kufanya tohara kwa hiari kwa wanaume.

Nyoni aliongeza kuwa SITETEREKI imebuniwa kama jukwaa la mawasiliano lenye utayari. Kwa sasa, SITETEREKI inalenga maeneo yatakayoonesha mafanikio makubwa katika kuboresha maisha, afya na ustawi wa vijana wa Kitanzania wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24 kwa kuwa takwimu zinaonyesha kuwa maambukizi ya VVU na mimba zisizotarajiwa huchangia kwa kiasi kikubwa vijana kuwa na afya duni, na vifo vya vijana.

‘Uhamasishaji wa SITETEREKI utafanyika katika ngazi ya jamii kupitia majadiliano katika vikundi vidogo yatakayoendeshwa na waelimishaji vijana, programu za redio za kijamii zilizoandaliwa kwa kushirikiana na vijana, pamoja na maigizo-jamii yaliyoandaliwa na vijana. 

Hata hivyo, shughuli hizi zitahusisha vijana kwenye majadiliano ya vikundi kuhusu vipaumbele muhimu vya tabia zinazohamasishwa, mabadiliko ya tamaduni, majadiliano juu ya vikwazo na fursa, zikioanishwa kupitia vyombo vya habari ili kusisitiza jumbe muhimu kwa vijana. Yote haya yatawafanya vijana wajione kitu kimoja, na kuwajengea uwezo na ujasiri wa kuwa na tabia chanya za kiafya’ Nyoni alisema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com