Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KAMPUNI YA VEGRAB ORGANIC FARMING LTD YAZINDUA SOKO LA PILIPILI KICHAA SINGIDA


 Mkurugenzi wa Kampuni ya Vegrab Organic Farming LTD,Gladness Nyange,akizungumzia kilimo cha pilipili kichaa wakati wa uzinduzi wa zao hilo uliofanyika Kitongoji cha Kipunda,Kjiji cha Mtunduru,wilaya ya Ikungi, mkoani Singida mwishoni mwa wiki.
 Afisa Ushirika wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi,Gurisha Msemo akizungumza kwenye uzinduzi huo.

Mwenyekiti wa Kipunda AMCOS, Omari Nyuda, akizungumza kwenye uzinduzi huo.
 Zao la pilipili baada ya kuvunwa.
 Zao la pilipili baada ya kuvunwa.
 Wakulima wa zao la pilipili wakiwa shambani.
 Mkulima Mohemed Salehe,  akizungumzia kilimo hicho.
Mkulima Mwanaidi Iddi, akizungumzia kilimo hicho.


Na Jumbe Ismailly,  Ikungi

KAMPUNI ya  Vegrab Organic Farming LTD kwa kushirikiana na kampuni inayouza matrekta ya AGRI-COM wamezindua soko la zao la pilipili kichaa litakaloweza kuwaongezea kipato wananchi wa Kitongoji cha Kipunda,Kjiji cha Mtunduru,wilaya ya Ikungi,Mkoani Singida.

Mkurugenzi wa Kampuni hiyo,Gladness Nyange alifafanua kwamba masoko ya zao la pilipili kichaa ni makubwa sana isipokuwa kinachotakiwa ni uzalishaji mkubwa na wenye ubora zaidi.

“Mimi nina imani na zao hili nyie mnaliona hivi lakini ni zao ambalo litatupeleka mbali sana kupitia juhudi ile tuliyoanzanayo tuendelee nayo,kwani masoko ni makubwa sana lakini yanataka uzalishaji mkubwa lakini pia wenye ubora.”alisisitiza Mkurugenzi huyo.

Kwa mujibu wa Nyange Mkoa wa Singida unaweza kuwa kituo kikubwa sana cha uzalishaji wa zao la pilipili kichaa na siyo kwa Tanzania tu bali hata kwa Afrika Mashariki na kwamba endapo wataweka jitihada wanaweza kuongoza katika Afrika katika uzalishaji wa zao hilo.

Hata hivyo Mkurugenzi huyo alifafanua kuwa mazingira pamoja na ardhi iliyopo katika Mkoa wa Singida inadhihirisha wazi kabisa kwamba pilipili itakayozalishwa kwenye maeneo yote ya Mkoa wa Singida itakuwa nzuri kuliko inayotoka sehemu yeyote ile ya Tanzania na hata Afrika Mashariki.

Akizindua mnada wa soko hilo la pilipili kichaa,Afisa ushirika wa Halmashauri ya wilaya ya Ikungi,Gurisha Msemo alisema Kampuni inayonunua zao hilo imesaini mkataba wa miaka mitatu na kwa msimu wa 2019/2020 kampuni hiyo itanunua pilipili kichaa iliyoiva kwa bei ya shilingi 4,500/=kwa kilo moja na shilingi 5,000/= kwa pilipili mbichi kwa kilo moja.

Aidha Msemo alitoa sababu za soko la zao hilo kuzinduliwa katika Kata ya Mtunduru kuwa ni kutokana na idadi kubwa iliyopo ya wakulima wa zao hilo ambapo kati ya wakulima 159 waliolima pilipili kichaa Mkoani Singida,110 ni wakulima kutoka wilaya ya Ikungi.

Akimkaribisha kuzindua soko hilo,Mwenyekiuti wa Kipunda Amcos,Omari Nyuda huku akitumia kauli mbiu isemayo ongeza tija pilipili inalipa,alisisitiza juu ya uzalishaji bora wa zao hilo ili waweze kuendelea kupata fedha nyingi zaidi.

“Zao hili ambalo limekuwa na tija kwetu na kauli mbiu tunasema ongeza tija pilipili inalipa mradi na msimu umeshazinduliwa,kwa hiyo yetu ni mapesa,tupate pesa tuongeze uzalishaji tuongeze zao ubora zaidi tuweze kusonga mbele zaidi.”alifafanua Nyuda ambaye ni mwenyekiti wa Kipunda Amcos.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com