Na John Walter-Manyara
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani Simanjiro mkoani Manyara kwa kushirikiana na jeshi la polisi wilayani humo, imemfikisha katika Mahakama ya Wilaya ya Simanjiro Afisa Mtendaji wa kata ya Langai Anna John Mlomi kwa makosa ya kudai na kupokea rushwa ya shilingi 100,000.
Taarifa iliyotolewa leo ijumaa juni 19,2020 na mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Manyara Holle Makungu imeeleza kuwa, kosa hilo ni kinyume na kifungu cha 15 cha sheria ya kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007.
Makungu amesema mwingine aliyeunganishwa katika mashtaka hayo ni afisa mtendaji wa kijiji cha Langai Masiar Sambana ambao walifikishwa mahakamani hapo na mwendesha mashtaka wa jeshi la polisi Magira Marwa na kufunguliwa kesi ya jinai namba CC 50 ya mwaka 2020.
Amesema baada ya kusomewa makosa yao mbele ya hakimu wa mahakama hiyo Onesmo Nicodemo, watendaji wote wawili walikana kupokea rushwa hiyo.
Taarifa ya mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Manyara imeeleza kuwa hadi wanaondoka mahakamani hapo ,washtakiwa walikuwa hawajatimiza masharti ya dhamana yaliyowekwa na mahakama.
Aidha uchunguzi wa TAKUKURU kuhusu shauri hilo umekamilika na kesi hiyo itatajwa tena mahakamani hapo Julai 1,2020.
Makungu ametoa rai kwa watumishi wa Umma mkoani Manyara na Tanzania kwa ujumla, kwamba ili kujiepusha na mkono wa sheria, wafanye rejea kwenye maandiko ya vitabu vitakatifu ikiwemo Quran na Biblia ambapo katika kitabu cha biblia Luka 3:12-14, watumishi wanaohusika na ukusanyaji wa maduhuli ya serikali waliagizwa kutotoza kuliko walivyoamriwa na kwa watumishi wote wakatakiwa kutosheka na mishahara yao. Kwa wale wanaokaidi yaliyoandikwa katika vitabu vitakatifu wafahamu kuwa mamlaka ziliwekwa na Mungu, hivyo wataendelea kupambana na mkono wa sheria.
Social Plugin