Ikiwa ni takribani siku 30 baada ya uteuzi wake kutenguliwa mnamo Mei 3, mwaka huu, aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Bohari ya Madawa nchini (MSD), Laurean Bwanakunu anashikiliwa kupisha uchunguzi kutokana na tuhuma za rushwa zinazomkabili.
Bwanakunu anashikiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru) makao makuu kuanzia leo Juni 2, 2020 pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Lojistiki wa MSD, Byekwaso Tabura.
Watuhumiwa wote wawili wapo mahabusu katika ofisi za taasisi hiyo zilizopo Upanga jijini Dar es Salaam kuanzia leo Juni 2, 2020 kupisha uchunguzi.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo Juni 2, 2020 na Afisa Uhusiano wa Takukuru Makao Makuu, Doreen Kapwani, watuhumiwa hao wanakabiliwa na tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia Serikali hasara kinyume na Sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa Namba 11 ya mwaka 2007.
Ikumbukwe kuwa Mei 3, mwaka huu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli alitengua uteuzi wa mkurugenzi huyo (Bwanakunu) na kumteua Brigedia Jenerali Dkt. Gabriel Mhidize kuwa Mkurugenzi Mkuu mpya wa MSD.
Social Plugin