MKUU WA MKOA WA RUKWA BWANA JOACHIM WANGABO
Mkuu wa Mkoa Rukwa Bwana Joachim Wangabo, ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani humo kuwakamata watumishi watatu wanaodaiwa kutafuna fedha mbichi za makusanyo ya ndani ya Sh milioni 27.6.
Kati ya Watumishi hao, mmoja anadaiwa kutafuna Sh milioni 4.5, mwingine Sh. milioni 8.4 na mwingine Sh. milioni 9.7.
Mkuu huyo wa mkoa pia amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, Missana Kwangura, kuwachukulia hatua kali za kinidhamu watumishi wote wanaodaiwa kutafuna fedha mbichi zaidi ya Sh milioni 53, ambazo ni makusanyo ya ndani ya halmashauri hiyo.
Kwangura alitoa maagizo hayo wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika jana mjini Namanyere, wilayani Nkasi, kujadili hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) za mwaka wa fedha 2018/2019.
Taarifa ya hoja za CAG ilibainisha kuwa, katika mwaka wa fedha 2018/2019, makusanyo ya ndani kiasi cha Sh milioni 47.7 yalikuwa hayajawekwa benki na baada ya ufuatiliaji hadi mwisho wa mwaka huo wa fedha, kiasi hicho kilipungua na kubaki Sh milioni 27.6, ambazo hazikuwasilishwa benki.
“Hiyo ni kinyume cha kifungu namba 50 (5) cha Sheria za Fedha za Serikali za Mitaa cha 2009 kinachoeleza fedha zote zilizokusanywa zipelekwe benki kila siku au siku inayofuata,” inaeleza sehemu ya taarifa ya CAG.
Alisema licha ya taarifa hiyo ya CAG kuonesha kuwa Sh milioni 27.6 ndio hakijapelekwa benki hadi mwisho wa mwaka wa fedha 2018/2019, lakini taarifa alizonazo zinaonesha hadi kufikia Mei 31, mwaka huu, kiasi hicho cha fedha kimeongezeka hadi kufikia zaidi ya Sh milioni 53.
“Hawa wanatupa shida sana wanakusanya mapato ya ndani, lakini badala ya kuzipeleka benki wanazila zikiwa mbichi, katika mkoa wetu imekuwa sawa na ugonjwa wa saratani ambao hauna dawa huku DED (Missana Kwangura) na madiwani wote mpo,” alisema.
Amesema fedha za makusanyo ya ndani ndiyo roho ya halmashauri yoyote ile ikiwamo ya Nkasi, hivyo hazipaswi kuchezewa.
Social Plugin