Mkurugenzi Rasilimali Watu na Utawala wa Benki ya Posta Tanzania (TPB), Diana Myonga (wa tatu kushoto) akimkabidhi Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Mkoa wa Singida, Aysharose Mattembe (wa nne kutoka kushoto) moja ya bati kati ya 100 yaliyotolewa mwishoni mwa wiki na benki hiyo kwa ajili ya kupaua madarasa ya shule mkoani humo. Kutoka kushoto ni Kaimu Meneja Mwandamizi wa Uhusiano wa benki hiyo, Chichi Banda, Meneja wa TPB Tawi la Singida, Redemter Rweyemamu. Wengine ni Wenyeviti wa Vikundi vya Wajasiriamali Manispaa ya Singida pamoja na wafanyakazi wa benki hiyo Mkoa wa Singida.
Mkurugenzi Rasilimali Watu na Utawala wa Benki ya Posta Tanzania (TPB), Diana Myonga (katikati) Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Mkoa wa Singida, Aysharose Mattembe (kulia) pamoja Kaimu Meneja Mwandamizi wa Uhusiano wa benki hiyo, Chichi Banda wakibadilishana mawazo wakati wa makabidhiano ya mabati hayo.Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Mkoa wa Singida, Aysharose Mattembe (aliyekaa katikati) , akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa benki hiyo baada ya kupokea msaada huo.
Picha ya pamoja na wajasiriamali.
Na Dotto Mwaibale, Singida
OFISI ya Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Mkoa wa Singida, Aysharose Mattembe imepokea mabati 100 kutoka Benki ya Posta Tanzania (TPB) kwa ajili ya kumalizia baadhi ya shule za msingi na sekondari mkoani hapa.
Akizungumza katika hafla ya kupokea msaada huo iliyofanyika viwanja vya benki hiyo mjini Singida mwishoni mwa wiki, Mattembe aliushukuru uongozi wa benki hiyo chini ya Mkurugenzi wake, Sabasaba Moshingi na kupongeza maboresho makubwa yaliyofanyika katika benki hiyo.
Alisema, TPB ni benki ya kizalendo kwani huduma zake zinalenga katika kuwakomboa watanzania kuanzia wale wa kipato cha chini kabisa hasa wajasiriamali hadi wale wa kipato cha kati.
Mattembe alisema mbali na hilo, benki hiyo imekuwa karibu sana wananchi wa mkoa wa Singida na ni mdau mkubwa katika kuunga jitihada za maendeleo za serikali ya awamu ya tano.
"Msaada huu sio wa kwanza hapa kwetu, nilishawahi kuwaomba vitanda vya kulalia wagonjwa kwenye Hospitali yetu ya Rufaa ya Mkoa wa Singida wakatupatia, wamekuwa wakitusaidia mara kwa mara nawashukuru sana. Naomba mnifikishie salamu zangu kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Posta, Sabasaba Moshingi na timu yake nzima kwa kazi nzuri ya kuifanya benki hii kuwa miongoni mwa taasisi bora za kifedha kwenye Ukanda wa Afrika Mashariki ..hongereni kwa kazi nzuri." alisema Mattembe.
Katika hatua nyingine Mattembe aliwaomba wananchi wa Mkoa wa Singida kuendelea kuiunga mkono benki hiyo kwa kufungua akaunti ili wapate huduma bora za kifedha na kuwa msaada huo utakwenda kusaidia kuboresha miundombinu ya shule mkoani humo.
Mkurugenzi Rasilimali Watu na Utawala wa TPB, Diana Myonga ambaye alikabidhi msaada huo kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa benki hiyo alisema msaada huo umekuja kwa wakati muafaka kwani shule zinatarajiwa kufunguliwa Juni 29, 2020 na kuwa kwa shule zile ambazo zimeombewa mabati hayo zitaezekwa na watoto wetu kusoma katika mazingira bora.
Myonga akizungumzia mafanikio ya benki hiyo alisema sasa ina matawi zaidi 28 nchi nzima na kuwa wanatoa huduma za kibenki kwa mawakala 151 wa Shirika la Posta na Simu na kuwa huduma zao zinawanufaisha hata wakulima wa vijijini tofauti na benki zingine zinazoishia mjini.
"Benki yetu imepiga hatua kubwa katika kuongezeka kwa mtandao wa utoaji huduma kutoka tawi moja hadi kufikia matawi 28 pamoja na kuifanya kutoa huduma za kisasa zinazoenda na wakati.
Myonga aliongeza kuwa benki hiyo inatoa huduma za haraka kwa wateja wake na zilizo nafuu ukilinganisha na benki zingine hivyo aliwaomba wananchi kujitokeza na kujiunga na benki hiyo ya kizalendo ambayo inamilikiwa kwa asilimia kubwa na Serikali.
Mkurugenzi huyo katika makabidhiano hayo aliambata na Kaimu Meneja Mwandamizi wa Uhusiano wa benki hiyo, Chichi Banda na Meneja wa TPB Tawi la Singida, Redemter Rweyemamu.
Wengine waliohudhuria makabidhiano hayo ni Wenyeviti wa Vikundi vya Wajasiriamali Manispaa ya Singida pamoja na wananchi.
Social Plugin