Wizara ya Afya ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imetangaza kuwa, homa ya Ebola imeripotiwa tena katika maeneo ya kaskazini magharibi mwa nchi. Taarifa hiyo imesema tayari watu wanne wameaga dunia katika siku chache zilizopita kwenye maeneo hayo kutokana na homa ya virusi vya Ebola.
Wizara ya Afya ya Congo DR imeongeza kuwa Taasisi ya Taifa ya Uhakiki wa Biomedical (INRB) imethibitisha kuwa, watu kadhaa waliofanyiwa vipimo katika mji wa Mbandaka wamepatikana na homa ya virusi vya Ebola.
Miezi miwili iliyopita Mkurugernzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) alitahadharisha kuhusu uwezekano wa mlipuko wa virusi vya homa ya Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Wimbi la maambukizi ya homa ya virusi vya Ebola lilianza tarehe 8 mei mwaka 2018 katika mji wa Bikoro mkoa wa Équateur uliko kaskazini magharibi mwa Congo DR na baadaye ikasambaa kwa kasi katika mji wa Mbandaka ambao ni makao makuu ya mkoa huo na mashariki mwa nchi hiyo.
Virusi hivyo vimesababisha vifo vya watu wasiopungua 2,200.
Social Plugin