Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

UMEMEJUA WAPIGA JEKI ELIMU SHULE YA SEKONDARI MORETO


Na Nyamiti Kayora

Shule nyingi za Sekondari hususani za vijijini zimekuwa zikikabiliwa na ukosefu wa nishati ya kuendesha maabara na mwanga wa kujisomea kwa wanafunzi waishio katika mazingira ya shule (bweni).



Uhaba huo umesababisha maeneo hayo kutofanya vyema kimasomo kuliko wale wenye nishati hiyo.

Shule zinazojiweza zimeweka umemejua wakati baadhi ya zile zisizokuwa na uwezo huo hasa za umma zimekuwa zikifadhiliwa na wahisani mbalimbali kama ilivyo shule ya sekondari Moreto. Shule hii ya sekondari Moreto ambayo ni ya bweni iko kwenye kijiji cha Mindutulieni,wilayani Chalinze mkoani Pwani.

Shule hii ilianzishwa na Chifu wa kabila la kimasai Moreto Lapa aliyekuwa akiongoza ukoo wa kimasai na jamii nzima ya kifugaji kwa mikoa ya Dar es Salaam na Morogoro.

Chifu Moreto alitoa wazo la kujenga shule na alihamasisha wanakijiji kujenga madarasa manne kisha Serikali ikaendeleza ujenzi na kuifanya shule kuwa na madarasa 13 ili kukidhi mahitaji ya mwingiliano wa jamii ya wafugaji na wakulima kijijini hapo.

Tangu kuanzishwa kwa shule hii mwaka 2011, haikuwahi kuwa na nishati yoyote ya umeme hadi mwaka 2017 ilipopata umeme jua.

Kazi kubwa ya umemejua shuleni hapo ni kuendesha maabara kwa masomo ya sayansi, kuwaangazia wanafunzi kwenye mabweni wakati wakijisomea masomo ya jioni baada ya kukamilisha vipindi vya darasani.

Vilevile umemejua huo umewezesha mazingira ya walimu kuishi shuleni hapo.

Moja kati ya wanafunzi waliohitimu mwaka 2019, Jacob Ibrahimu anasema walikuwa wakitumia tochi tangu alipoanza kidato cha kwanza hadi cha tatu hali ambayo iliwafanya baadhi kuacha shule kwa kukosa pesa za kununua betri.

“Tulikuwa tunatumia vitochi, hali hii iliwafanya wengine kutokuhudhuria darasani, ila tulipofika kidato cha tatu ndipo wakaleta sola, walimu waliongezeka na walianza kutufundisha masomo ya sayansi kwa vitendo katika maabara,” alisema Jacob.

Mbali na kuepusha gharama za betri na wanafunzi kuacha shule, umemejua huo umefanya wanafunzi waanze kufaulu masomo.

Janeth Ibrahimu mwanafunzi shuleni hapo anabainisha kuwa umemejua uliowekwa shuleni kwao umewasaidia kuongeza ufanisi katika masomo yao hasa kwa masomo ya sayansi.

“Sasa tunasoma masomo ya sayansi vizuri , lakini bado umeme unaleta changamoto mvua zikifululiza hivyo, tunaomba serikali ituwekee mazingira ya kupata umeme wa uhakika,”alisema Janeth.

Makamu mkuu wa shule ya Moreto mwalimu Ngasa Charles Madata anasema umemejua huo walioupata kupitia wadau wa nishati jadidifu shirika la Innovation Afrika 2017,umesaidia wanafunzi kuachana na kadhia ya kujisomea kwa kutumia tochi za betri hali iliyoathiri maendeleo ya kielimu hasa katika mitihani ya kidato cha nne .

“Hali ya ufaulu ilikuwa chini sana na wanafunzi wengi walikuwa wakiacha shule,ila baada ya ujio wa hizi sola, utoro umepungua na ufaulu ulianza kujitokeza mwaka huo huo wa 2017,” alisema Mwalimu Mdata.

Kwa mjibu wa Takwimu za matokeo ya kidato cha nne toka Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) wanafunzi 32 walifaulu mwaka 2016 kati ya 60.

Mwaka 2017 wanafunzi 33 walifaulu kati ya wanafunzi 67.

Huku mwaka 2018 walifaulu wanafunzi 34 kati ya 53.
Aidha mwaka 2019 walifaulu wanafunzi 51 kati ya 70 ikiwa ndiyo ufaulu wa juu kufikiwa ndani ya muda mfupi.

Licha ya ongezeko la wanafunzi kufaulu shuleni hapo, na kupenda kusoma masomo ya sayansi kutokana na maabara iliyopo kuanza kufanya kazi mwaka 2019,imeelezwa bado wanakumbana na changamoto ya kuwa na chumba kimoja cha maabara kinachopelekea masomo yote ya sayansi yafanyike humo.

“Tangu kuanza kutumika kwa maabara mwanafunzi wengi wanatamani kusoma masomo ya sayansi,na hali hii inatupa shida kidogo kufanya practical za masomo hayo hasa pale zinapofatana mana tuna maabara moja,”aliongeza mwalimu Madata.

Pia Umemejua shuleni hapo umewafanya angalu walimu wavutike kuendelea kufundisha.

“Tangu tumepata umeme nimehamia shuleni hapa,ingawaje umeme wetu huu si wa kudumu lakini navutika hata kuwafundisha wanafunzi usiku,” aliongeza Mwalimu Hamisi.

Jamii ya Kijiji cha Mindutulieni pia wanaona fahari ya uwepo wa umemejua katika shule ya Moreto unaonyesha matumaini kwa elimu ya watoto wao.

Furaha yao kubwa ni kuona ufaulu kwa watoto wao ukiongezeka na kuwapa chachu wanafunzi kusoma masomo ya sayansi wanayoamini miaka ya mbeleni watapa wataalumu wengi wa kisayansi kijiji hapo.

Moja kati ya wazazi kijijini hapo Magreth Katei anasema amefurahi kupunguziwa mahitaji ya mwanafunzi awapo shule na amefarijika mwanae kusoma masomo ya sayansi.

“Sola zimetupunguzia gharama sisi wazazi, sahivi hatununui tena tochi wala betri,pia mwanangu anasema kuna mabara hivyo anasoma sayansi, yani namuombea awe Daktari ili aje atusaidie katika familia,” alisema Magreth.

Pamoja na furaha hiyo bado wazazi wanatamani kupata umeme kijijini kwao ili watoto wanapofunga shule wawe na uhakika wa kujisomea nyumbani.

“Tunatamani sana kupata umeme huku majumbani, kwani watoto wakifunga shule ni changamoto, unakuta tunatumia tochi moja sijui upikie jikoni mtoto naye anataka kusoma, kweli hapa inakuwa shida,”aliongeza Magreth.

Naye Deogratius Shayo, Mwenyekiti wa bodi ya shule ya sekondari Moreto anasema mwaka 2015 ndo alishika wadhifa huo na kulikuwa na changamoto ya umeme hivyo kitaaluma ingeshuka tu kwani wanafunzi wasingeweza kufanya vizuri katika mazingira ya giza.

“Kwa kweli tangu tumepata umeme Watoto wanaelewa, na walimu wamejitolea kufundisha muda wa ziada hasa wanafunzi wa kidato cha pili na nne kwa kuwajengea uwezo zaidi na ufaulu kweli umeongezeka,” alisema Shayo.

Wachambuzi wa masuala ya elimu wanasema ufaulu wa mwanafunzi hautegemei umeme tu, bali hata mazingira tulivu anapoishi, uwezo na malezi,ingawa kwa miaka ya sasa umeme unatajwa kuwa muhimu zaidi hasa kwa masomo ya Sayansi.

Profesa Omary Minz kutoka chuo cha Muhimbili anabainisha kuwa, shule zenye changamoto ya kutokuwa na umeme wa Grid ya Taifa watumie nishati jadidifu ili kusaidia ufanisi wa ufaulu wa masomo ya sayansi.

“Uwepo wa umeme katika shule za sekondari ni muhimu na ni muhimu kupindukia hasa katika kufanikisha masomo ya sayansi yanayomtaka mwanafunzi kutumia maabara kusoma kwa vitendo,”alisema Prof. Minz.

Si kufaulu tuu katika masomo ya sayansi bali Profesa Minz aliongeza kuwa mwanga shuleni unasaidia pia kumpatia chachu mwanafunzi kusoma kwa bidii nyakati za usiku au alfajiri ambapo wengi wamepumzika na mazingira kuwa na utulivu.

“Sisi tulikuwa tunaamka usiku kujisomea, unalala saa nne usiku kwenye saa kumi alfajiiri kale ka utulivu unaamka akili ikiwa imetulia unasoma, sasa kama hakuna mwanga hata wa sola kwa kweli ufaulu kwa wanafunzi utausikia kwa wachache,”aliongeza Prof. Minz.

Kufuatia hali hii inayoleta tija ya utumiaji wa nishati jadidifu ya mwanga wa jua, makamu mwenyekiti wa jumuiya ya wazalishaji wa nishati hizi Tanzania, mhandisi Prospel Magali ambaye pia ni mkurugenzi wa miradi ya ENSOL Tanzania anasema umemejua umekuwa mkombozi wa shule nyingi nchini Tanzania.

Magali anasema taasisi nyingi zilizo pembezoni mwa miji na ambazo hazijafikiwa na umeme wa grid ya taifa zimekuwa zikinufaika na nishati jadidifu.

Amesisitiza pia watumiaji wa nishati jadidifu wanao wajibu wa kuchagua vifaa vyenye ubora na kuzingatia makadilio sahihi ya matumizi ya umemejua na vifaa gani na vitumikeje.

Aidha aliongeza kuwa mtuaji azingatie Makadilio sahihi ya kitaalamu ya mfumo wa umemejua unaoendana na matumizi sahihi ya umeme.

Hata hivyo amesema nishati jadidifu zimekuwa mkombozi kwa shule nyingi ambazo sasa zinaendesha masomo ya sayansi kutumia maabara na kuongeza chachu ya ufaulu kwa wanafunzi akitolea mfano shule ya msingi Mpale iliyopo wilayani Korogwe mkoani Pwani ambayo imefaidika na umeme jua toka kampuni ya ENSOL uliochangiza ufaulu shuleni hapo.












Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com