Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Dar es Salaam, Mussa Kilakala (kushoto), akiwa na Mkuu wa Mkoa huo, Paul Makonda kwenye kikao cha Baraza la UVCCM katika Ukumbi wa Anatoglo
Na Mwandishi wetu ,Dar
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amewataka Vijana wa Chama cha Mapinduzi (CCM), kukilinda chama hicho na kuyaeleza maendeleo yaliyofanywa na Rais Dk. John Magufuli katika kipindi cha miaka mitano.
Makonda alitoa kauli hiyo wakati wa kikao na Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM), Mkoa wa Dar es salaam ambapo amesema yapo maendeleo makubwa yaliyofanywa na Serikali ya awamu ya tano na kama wasipoyazungumzia watatoa mwanya kwa watu wasiolitakia mema taifa kupenyeza uongo.
“Yapo mambo mengi amabayo yamefanywa na Serikali na ninyi vijana mnayajua bila hata kuelekezwa msipoyasema iko siku wasioitakia mema nchi hii watayageuza na kuwa mabaya hivyo ni jukumu lenu kuwaeleza wananchi,” amesema Makonda.
Makonda amesema vijana wa Mkoa wa Dar es Salaam wasisubiri kupewa posho na maelekezo namna ya kukisemea chama hicho bali wajitume kwa ukeleketwa wao na kukipigania chama hicho.
“Sisi tulikuwa tukienda kuomba vipindi katika televisheni mbalimbali kuwajibu wanaokitukana chama huku tukiwa hatuna vyeo vyovyote tukiulizwa tunajibu kuwa sisi ni makada si kila kitu usubiri kutumwa, kupokea maelekezo,” amesema Makonda.
Amesema kwa mujibu wa kanuni vijana wa CCM ndio walinzi wa chama hivyo wanajukumu kubwa la kuhakikisha hakuna mtu anayeweza kukisema vibaya wala kukishambulia.
“Vijana wa sasa wa CCM wamekuwa wakiwasaidia kusambaza ujumbe wanaoitukana serikali na kusambaza uongo katika makundi na kulalamika kuwa anahitaji kujibiwa, ajibiwe na nani wakati wewe ni kijana wa ccm,” amesema Makonda.
Makonda amewataka kuwatambua na kusaidia watu wenye vipaji vya uongozi wanaohitaji nafasi mbalimbali za uongozi katika Uchaguzi Mkuu.
“Tambuanaeni na mheshimiane kwa vipaji na uwezo ambavyo Mungu ameviweka ndani yenu na wasaidieni ambao wanaomba uongozi mkijua wana uwezo wa kuongoza,” amesema Makonda.
Aidha Makonda amewataka vijana hao kuwa macho hususani kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu kwakuwa wapo baadhi ya watu wenye tamaa watakuwa tayari kuvunja hata amani ili tu wapate fedha za kushibisha matumbo yao.
Ameahidi kuanza ziara na kamati ya siasa ya mkoa ifikapo Juni 20, mwaka huu kwa lengo la kukabidhi kwa chama miradi yote iliyotekelezwa na Serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais Magufuli.
Makonda alitoa msaada wa mabati na mbao za kupaua kwaajili ya kukamilisha ujenzi wa ofisi ya UVCCM Wilaya ya Kigamboni.
Amesema ametoa vifaa hivyo vya ujenzi kwa kuwa tayari Kigamboni wameanza ujenzi.
Kwa upande wake Mwenyeti wa UVCCM Mkoa wa Dar es Salaam, Mussa Kilakala, amesema kuwa CCM katika mkoa huo haina mjadala katika kushinda kwa kishindo kikuu kutokana na utekelezaji boravwa ilani katika kipindi cha miaka mitano.
“Ukweli ni kwamba Rais Magufuli anawajua watu anaowaongoza na najua hali zao, Dar es Salaam tutashinda kwa kishindo, mwaka 2015 tunajua hatukufanya vizuri katika kumpigia kura lakini kwa kutambua kuwa maendeleo hayana chama mkoa huu ndiyo unaoongoza kwa miradi mingi mikubwa ya kimkakati,” amesema Kilakala.
Social Plugin