Waziri Kairuki akizungumza na wafanyakazi wa kampuni ya Qwihaya alipofanya ziara kiwandani hapo.
Na Francis Godwin - Mufindi
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri mkuu -Uwekezaji Angellah Kairuki ameeleza kufurahishwa na kasi ya uwekezaji inayofanywa na kampuni ya uchakataji nguzo za umeme ya Qwihaya General Enterprises Company Ltd kwa kuwekeza viwanda vya nguzo katika mikoa mbalimbali ukiwemo mkoa wa Kigoma na kutaka wadau wengine kuelekeza nguvu zao katika mkoa wa Kigoma badala ya kuwekeza Dar es Salaam ,Dodoma na mikoa mingine ambayo ni rahisi kufikika.
Waziri Kairuki alitoa pongezi hizo jana baada ya kufanya ziara katika kampuni hiyo Mjini Mafinga ambapo alisema kuwa mkoa wa Kigoma ni mkoa ambao upo pembezoni na shabaha ya serikali ni kuendelea kuhamasisha na kuwavutia wawekezaji wengi zaidi kufika kuwekeza viwanda katika mkoa huo badala ya kuona uwekezaji mkubwa ukifanyika Dar es Salaam ,Arusha ,Mwanza na mikoa mingine ambayo kimsingi ni rahisi kufikika .
Alisema kuwa mkoa wa Kigoma upo pembezoni mwa nchini na wawekezaji wengi wamekuwa wakikwepa kuwekeza viwanda vyao katika mkoa huo kutokana na umbali ila kampuni hiyo ya Qwihaya imeweza kufika na kuwekeza kiwanda ndani ya mkoa wa Kigoma ,Njombe na Iringa jambo ambalo ni jema na la kupongezwa zaidi.
"Kitendo cha Qwihaya kufika kuwekeza Kigoma ni uzalendo wa hali ya juu na mmefungua mlango kwa wawekezaji wengine kufika kuwekeza katika mkoa wa Kigoma maana nako kuna watanzania ambao wanahitaji kunufaika na sekta ya uwekezaji sio kwamba siwapongezi kwa kuwekeza kiwanda hapa Mafinga mkoani Iringa nawapongeza pia ila kwenda Kigoma mmefanya jambo zuri zaidi maana kupitia mkoa wa Kigoma mtakuwa na uwezo wa kuuza bidhaa zenu katika nchi za jirani na Tanzania",alisema.
Pia Waziri huyo alisema mpango wa kampuni ya Qwihaya wa kufungua kiwanda cha kutengeneza dawa ya kutibu nguzo Kibaha ambacho kitakuwa ni kiwanda cha kwaza cha aina hiyo kwa Tanzania kwani alisema kwa sasa hakuna kiwanda cha dawa ya kutibu nguzo nchini .
Akizungumzia changamoto za miundombinu ya barabara ya Mgololo Mufindi alisema kuwa tayari TANROADS mkoa wa Iringa wamekwisha fanya upembuzi yakinifu juu ya barabara hiyo na wakati wowote itafanyiwa matengenezo ya kiwango cha lami .
Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa Kampuni ya Qwihaya Leonard Maheda alisema kiwanda hicho kimeanzishwa mwaka 2007 kama kiwanda cha uchanaji mbao na mwaka 2015 kilianza kutengeneza nguzo baada ya kauli mbinu ya Rais Dkt John Magufuli juu ya serikali ya viwanda na hata kuzuia nguzo kutoka nje ya nchi .
Alisema kiwanda hicho kwa mwaka kina uwezo wa kuzalisha nguzo 800,000 na kuwa nchi nzima wanamiliki viwanda vitatu vya nguzo na wanakusudia kuanzisha kiwanda cha dawa za nguzo ambacho kitakuwa kiwanda pekee cha dawa za nguzo Tanzania .
Awali akisoma taarifa ya kiwanda hicho kwa waziri Kairuki ,Kaimu Mkurugenzi wa kampuni ya Qwihaya General Enterprises Ltd Benedicto Mahenda alisema gharama za uwekezaji wa kiwanda hicho ni takribani kiasi cha shilingi bilioni 15.
Alisema kwa kipindi kirefu kampuni imekuwa ikinunua malighafi za nguzo kutoka katika shamba la miti la Sao Hill iliyopo chini ya TFS na wamekuwa wakipata ushirikiano mkubwa kutoka kwa uongozi wa shamba hilo .
Meneja huyo alisema soko la nguzo wamekuwa wakitegemea zaidi soko la ndani kupitia mteja mkubwa shirika la umeme Tanzania (TANESCO) na katika kipindi cha hiki cha utekelezaji wa mradi wa umeme vijijii (REA) awamu ya tatu) soko la nguzo limekuwa ni kubwa sana .