WANANCHI WATAKIWA KUIUNGA MKONO SERIKALI KWA KUBORESHA HUDUMA ZA MATIBABU YA KIBINGWA HAPA NCHINI


Wananchi wametakiwa kuiunga mkono Serikali kutokana na maboresho makubwa yaliyofanywa ya upatikanaji wa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo zinazotolewa hapa nchini.


Rai hiyo imetolewa jana jijini Dar es Salaam na  Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin Mollel  alipokuwa akizungumza na wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa ziara yake ya kikazi aliyofanya katika Taasisi hiyo  ya kuangalia huduma  za matibu ya moyo zinazotolewa.

Dkt. Mollel alisema miaka ya nyuma huduma nyingi za kibingwa hazikuwa zinapatikana hapa nchini na hivyo kuifanya Serikali kutumia fedha nyingi kulipia matibabu ya wagonjwa nje ya nchi lakini hivi sasa Serikali imewasomesha wataalamu wa kutosha, imejenga Hospitali za kisasa na kununua vifaa tiba vya kisasa na hivyo  wagonjwa wengi kutibiwa hapa nchini.

“Hivi sasa huduma za matibabu ya kibingwa hapa nchini zimeimarika, kwa upande wa wagonjwa wa moyo wanafanyiwa matibabu ya upasuaji wa kutumia tundu dogo linalotobolewa kwenye paja na upasuaji mkubwa wa kusimamisha moyo na wataalamu wa ndani huduma ambazo hazikuwa zinapatikana hapa nchini,”alisema Dkt. Mollel.

Naibu Waziri huyo alisema kazi za kuboresha sekta ya afya zinazofanywa na Rais Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli zimevuka hadi nje ya nchi ndiyo maana wagonjwa wanakuja kutibiwa hapa nchini  wakitokea  mataifa mbalimbali.

Pia kutokana na  madaktari bingwa wabobezi kuwa  wachache  na ili huduma hii  iweze kuwafikia wananchi wengi zaidi  Serikali imeanzisha program ya tiba mtandao ambayo itawasaidia  wagonjwa walioko mikoani kuweza kupata huduma hukohuko waliko bila ya kufuata huduma hizo Dar es Salaam.

“Kipindi hiki ambacho Dunia  inakabiliwa na janga la ugonjwa Corona mipaka ya nchi nyingi ilikuwa imefungwa watu hawakuwa wanasafiri kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine,  kwa kuwa   Serikali ilikuwa imeboresha huduma za matibabu ya kibingwa ya magonjwa mbalimbali huduma zote hizo zilikuwa zinapatikana hapa nchini na wagonjwa walikuwa wanaendelea  kutibiwa,” alisema Dkt.Mollel.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Prof. Mohamed Janabi alisema changamoto kubwa wanayoipata ni wagonjwa wengi kufika katika Taasisi hiyo wakiwa wamechelewa  huku mioyo yao ikiwa imechoka. Wagonjwa hao wakifanyiwa upasuaji mkubwa wa kusimamisha moyo wanatumia  chupa za damu sita hadi nane lakini kama wangewahi  wangeweza kutumia hadi  chupa mbili za damu.

Prof. Janabi alisema Serikali imefanya uwekezaji kubwa kwa kuanzisha Taasisi hiyo  kwani kabla haijaanzishwa wakati iko Kitengo cha magonjwa ya moyo ndani ya Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kipindi cha miaka saba mwaka 2008 hadi 2015 walifanya upasuaji wa moyo kwa wagonjwa 604 lakini baada ya kuanzishwa kwa mwaka 2016 hadi sasa  wamefanya  upasuaji kwa wagonjwa 1537.

“Tumefanya upasuaji mkubwa wa kusimamisha moyo na kupandikiza mishipa ya damu kwenye moyo (Coronary Artery Bypass Grafting-CABG) kwa wagonjwa 100 ambapo asilimia 92 walipona na asilimia nane walipoteza maisha. Tunashukuru tumeokoa maisha ya watanzania ambao hivi sasa wanaendelea na majukumu yao ya kazi za kila siku”, alisema Prof.Janabi.

Naye Mkurugenzi  Msaidizi wa huduma za Umma na Binafsi kutoka Wizara ya  Afya, Maendeleo ya Jamii ,Jinsia ,Wazee na Watoto Dkt. Vivian Wonanji alisema  wakati ambao nchi yetu inaelekea katika uchumi wa kati idadi ya watu wenye magonjwa yasiyo ya kuambukiza inaongezeka, hii ni kutokana na mfumo wa maisha ambao watu wanaishi .

“Mwaka jana Wizara ilizindua mpango wa kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ili kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya ufahamu ya magonjwa hayo. Kwa wale ambao wamepata magonjwa hayo yakiwemo magonjwa ya moyo Serikali itahakikisha wanapata huduma za matibabu na ambao hawana magonjwa hayo wanakuwa na uelewa wa kutosha ili waweze kuepuka kupata  magonjwa hayo”, alisema Dkt. Wonanji.

Naibu Waziri Mollel akiwa katika Taasisi hiyo alitembelea wodi ya watoto, Cathlab,  chumba cha upasuaji , wodi ya wagonjwa walioko katika uangalizi maalum, alizungumza na wagonjwa aliowakuta wanapata matibabu pamoja na wafanyakazi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post