Na. Aron Msigwa – WMU.
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla amesema kuwa Tanzania imejipanga na iko tayari kupokea watalii kutoka katika mataifa mbalimbali ikiwemo nchi ya Sweden na Israel ambazo raia wake wamekua wakitembelea vivutio mbalimbali vya utalii vya Tanzania.
Dkt. Kigwangalla ameyasema hayo leo jijini Dar es salaam wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Ulf Kallstig na Balozi wa Israel kwa Tanzania, Oded Joseph ikiwa ni mwendelezo wa mikutano yake na mabalozi wa nchi mbalimbali ambazo ni masoko makuu ya utalii kwa Tanzania.
Dkt. Kigwangalla amewaeleza mabalozi hao kuwa mikutano anayoifanya na mabalozi wa nchi mbalimbali inalenga kulinda uhifadhi na kujenga uelewa wa pamoja kuhusu hatua zilizochukuliwa na Tanzania kufungua Sekta ya Utalii wakati huu wa janga la Corona na kuwaomba mabalozi hao wawahamasishe na kuwashawishi raia wa nchi zao na makampuni ya utalii yaendelee kufanya biashara ya utalii na Tanzania.
Amewaeleza mabalozi hao kuwa Tanzania imekwisha fungua anga na kuruhusu ndege za abiria za kimataifa kutua hali iliyochangia kufunguka kwa Sekta ya Utalii Tanzania kutokana na utayari, mazingira salama na maandalizi mazuri ya kupokea na kuhudumia watalii watakaowasili nchini wakati huu wa janga la Corona.
Dkt. Kigwangalla amewaeleza mabalozi hao kuwa Tanzania imezindundua mwongozo wa Taifa wa uendeshaji wa shughuli za Utalii unaosimamia usalama na afya za wadau wote wanaojihusisha na sekta ya utalii wakati huu wa janga la Corona.
Amewahakikishia mabalozi hao kuwa watalii wote wanaowasili Tanzania katika kipindi hiki cha janga la Corona wako salama kutokana na uwepo wa mwongozo huo unaolinda afya za wasafiri kuanzia kuwasili na kuondoka kwao.
Dkt. Kigwangalla amesisitiza kuwa mwongozo huo unatoa usimamizi kwenye viwanja vya ndege, hoteli za kitalii, Watoa huduma za utalii, upimaji wa afya za wahudumu na wageni wote wanaoingia nchini pamoja na ukusanyaji wa taarifa za wasafiri wote wanaoingia nchini Tanzania.
Aidha, amewahakikishia mabalozi hao kuwa mifumo ya huduma za afya nchini imeimarika na iko tayari kuhudumia watalii watakaokuwa wakiwasili kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii akibainisha kwamba Tanzania ina hospitali za kisasa, maabara za upimaji zenye vifaa vyote na huduma za dharula kwa watalii watakaoshukiwa au kuonesha dalili za ugonjwa wa Corona.
Kwa upande wao mabalozi hao wakizungumza kwa nyakati tofauti wamemshukuru Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla kwa hatua na juhudi anazozifanya kuendeleza uhifadhi nchini na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali ya Tanzania katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za uhifadhi.
Katika juhudi zake za kuhamasisha na kufungua sekta ya utalii Waziri Kigwangalla ameshakutana na kuzungumza na mabalozi wa nchi mbalimbali ikiwemo Ujerumani, Israel, Sweden, Netherland na Finland.
MWISHO
Social Plugin