WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli itaendelea kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili Watanzania wote zikiwemo za afya, maji, miundombinu na elimu bila ya kujali itikadi zao.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatano, Juni 24, 2020) alipozungumza na wananchi baada ya kutembelea Zahanati ya kijiji cha Nandagala akiwa katika ziara ya kikazi wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi, ambapo amewataka wananchi washikamane na Serikali katika kuboresha maendeleo yao.
“Suala la maendeleo halina chama, maendeleo yaliyoletwa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi ni kwa ajili ya wananchi wote, hivyo watu wote tunatakiwa tushikamane kwa pamoja kumshukuru na kumuunga mkono Rais Dkt. Magufuli kwani shule, hospitali anazojenga zinatumika na watu wote.”
Amesema wananchi wanatakiwa watambue jitihada kubwa zinazofanywa na Rais Dkt. Magufuli katika kuboresha huduma za afya. “Leo nimeshuhudia wagonjwa wakiwa wamelazwa katika zahanati yetu ya Nandagala. Haya ni mafanikio makubwa awali hatukuwa na Zahanati hapa.”
Amesema awali kijiji hicho hakikuwa na Zahanati na wakazi wake waliuguzwa majumbani kwa kushindwa kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya, ujenzi wa zahanati hiyo umekuwa mkombozi mkubwa hususani kwa wajawazito kwani huduma zote zikiwemo za mama na mtoto zinatolewa hapo.
Vilele, Waziri Mkuu ametembelea kijiji cha Luchelegwa na amekabidhi gari la kubebea wagonjwa katika Kituo cha Afya cha kata ya Luchelegwa. Gari hilo limetolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa ufadhili wa Global Fund.
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwaagiza viongozi wa vijiji vyote ambavyo havina zahanati viongozi wake waanzishe miradi ya ujenzi wa zahanati na watakapokamilisha ujenzi wa maboma Serikali itawapelekea vifaa vya viwandani yakiwemo mabati na misumari.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Luchelegwa Dkt. Codratus Mutabihirwa ameishukuru Serikali kwa kuwapa gari la kubebea wagonjwa kwani awali walikuwa wanapata tabu pale wanapokuwa na mgonjwa anayetakiwa kuhamishiwa hospitali ya wilaya.
Amesema gari hilo litatumika kwa matumizi yaliyokusudiwa na kwamba watalitunza ikiwa ni pamoja na kuhakikisha linakuwa na mafuta wakati wote. “Tayari tumeshatenga fedha katika bajeti ijayo kwa ajili ya gari hili, hivyo hata matengenezo kinga yatakuwa yanafanyika kwa wakati.”
Nao baadhi ya wananchi wa kijiji cha Luchelegwa walitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali kwa kuwapatia gari la kubebea wagonjwa kwa sababu walikuwa wanapata tabu sana hususani kwa wajawazito ambao walikuwa wakihamishiwa hospitali ya wilaya kwani walikuwa wanatumia pikipiki.
Mmoja wa wananchi hao Sauda Kaisi amesema anaishukuru Serikali kwa kuwapelekea gari hilo kwa kuwa Kituo cha Afya cha Luchelegwa hakikuwa na gari la kubebea wagonjwa jambo ambalo lilisababisha baadhi ya ndugu zao kupoteza maisha kwa kushindwa kupata huduma kwa wakati.
Mkazi mwingine wa kijiji hicho Joyce Chimela amesema anamshukuru Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa uboreshaji wa huduma mbalimbali kwenye wilaya yao kikiwemo Kituo chao cha Afya cha Luchelegwa ambacho kimepewa gari la kubebea wagonjwa litakalowafikisha kwa wakati hospitali ya wilaya.
Mwisho.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
Social Plugin