Na Mwandishi Wetu, Pwani.
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amefanya ziara ya kushtukiza katika Shule ya Sekondari Bwawani ambayo inamilikiwa na Jeshi la Magereza na kubaini madudu ikiwemo magari ya Jeshi yamesajiliwa kwa namba binafsi.
Waziri Simbachawene alianza ziara yake kwa kutembelea Gereza la Kilimo Ubena na baadaye kuelekea katika shule hiyo ambazo zote zipo jirani ndani ya Kata ya Bwawani Mkoani Pwani.
Akizungumza na uongozi wa shule hiyo, Simbachawene alisema Sekondari hiyo ni mali ya umma lazima mali za shule hizo zisajiliwe kwa namba za Jeshi la Magereza zinazojulikana kwa kifupisho cha MT (Magereza Tanzania).
Alisema haiwezekani magari matatu ikiwemo ya Mkuu wa Shule hiyo imesajiliwa kwa namba binafsi, lori pamoja na gari lingine mali ya shule hiyo, kitendo hicho ni uvunjifu wa taratibu za serikali na anahitaji kupewa taarifa ya maandishi.
“Mkuu wa Gereza Ubena wewe ndio kiongozi hapa, nakuagiza umfikishie ujumbe CGP (Kamishna Jenerali wa Magereza), ifikapo kesho mchana nipate taarifa ya shule hii ikiwemo kwanini magari ya Jeshi yamesajiliwa kwa namba ‘private’ (binafsi), na pia nipate CV za walimu wa shule hii pamoja na watumishi wote,” alisema Simbachawene.
Aliongeza kuwa, “inawezekana shule hii ikawa nikijiwe fulani ambacho watu wanajipatia fedha, mpaka magari wanasajili kwa namba private ili wafanyie nini?, gari la serikali tunajua hata kama itakua inasomba mawe, lakini sio ajabu hiyo gari inafanya kibarua huko mtaani inafanya vibarua vya watu, inabeba matofali, unaitofautisha vipi na magari mengine, siwezi kuhukumu moja kwa moja naomba nipate taarifa ya maandishi kutoka kwa CGP kupitia kwako.”
Waziri Simbachawene kutokana na mapungufu hayo aliyoyaona, alitaka kujua zaidi ufaulu wa wanafunzi wanamaliza masomo yao, pia alitaka kujua mapato na matumizi ya shule hiyo ambayo amesema inamazingira mazuri, eneo zuri lakini uongozi umeshindwa kuiitangaza na haina umaarufu wowote hapa nchini.
Kwa upande wake Makamo Mkuu wa Shule hiyo, Solomon Mwambingu alisema shule hiyo ilianzishwa mwaka 1981, na kuhusu ufaulu inafanya vizuri kuanzia kidato cha nne hadi cha sita.
“Shule inafanya vizuri kitaaluma, matokeo ya kidato cha pili kwa mwaka jana 2019 wanafunzi wote walifaulu, pia kidato cha nne walifanya vizuri na matokeo ya kidato cha sita wanafunzi wote walifaulu na hakukua na hakukua na daraja zero wala daraja la nne,” alisema Mwambingu.
Aidha, Waziri Simbachawene kwa upande wa Gereza la Mifugo aliwapongeza kwa kutunza mifugo iliyopo katika gereza hilo, na kuwataka kuwepo na soko la nyama kwa kuchinja ng’ombe ili waweze kuuza na kupata mapato kupitia ufugaji wa kuvuna.
“Lazima magereza ijitegemee, gereza la mifugo halina hata nyama za kuuza, tunataka uchungaji wenye faida, kuwepo na ‘brandy’ yenu, mnaweza mkachukua mfuko mkaweka nyama na kuandika bwawani meat, na pia kuzalisha maziwa yakutosha, hivyo ndivyo kujitangaza,” alisema Simbachawene.
Pia aliwataka aliagiza kuwa, mifugo mbalimbali ng’ombe zichinjwe na nyama ziweze kutangazwa kwa kuwa na utambulisho maalumu ili kuliletea mapato Jeshi hilo kwa kuwa wana eneo hilo.
Kwa upande wake Msimamizi wa Shamba la Magereza katika Gereza hilo, Charles Masuka alisema shamba hilo lina ekari 12 ambapo wanafuga ngombe, mbuzi, kondoo na bata, hivyo shamba hilo linatoa ngombe wa nyama ambapo wanatoa kwa wahitaji.
“Tunashukuru kiongozi kwa kututembelea, ujuoio wake umetupa hamasa, na shmaba hili ni kubwa lina mifugo 2,335, shmaba hili linategemewa utoaji wa ngomnbe wa nyamba,” Masuka.
Simbachawene alimaliza ziara yake ya siku moja katika Gereza hilo, na aliwataka viongozi wa Gereza hilo wampe ushirikiano Mkuu wa Jeshi hilo, kwa kuwa na mipango mizuri ya kulipeleka mbele Jeshi hilo, na aliwataka waendelee kuchapa kazi zaidi pamoja na kuhakikisha wanajitegemea kwa chakula ili Magereza nchini yaweze kusonga mbele.
Social Plugin