Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI UMMY AITAKA BODI MPYA YA TMDA KUWEZESHA UKUAJI WA UCHUMI NA USHAMIRI WA BIASHARA NA UWEKEZAJI TANZANIA

Na WAMJW-DODOMA

Bodi mpya ya ushauri ya Wizara ya Afya kwa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imetakiwa kuisimamia mamlaka hiyo na kuacha kufanya kazi ya kipolisi kwa wenye viwanda vidogo na vya kati na bali kuwawezesha kushamiri kwa biashara na uwekezaji nchini Tanzania.

Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu alipokuwa akizundua bodi hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti Bw. Eric Shitindi Jijini Dodoma.

“Nimekuwa nikieleza TMDA haipaswi kufanya kazi ya kipolisi hususani kwa wenye viwanda vidogo na vya kati, mnapochukua maamuzi haya mnatakiwa mjiulize je yanachangai kuwezesha uendelevu wa uwekezaji au biashara katika ukuaji wa uchumi wa viwanda?” amehoji Waziri Ummy Mwalimu.

Amesema jukumu kubwa la TMDA ni kulinda afya ya jamii kwa kudhibiti ubora, usalama na udhibiri wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi na kuwataka wasiongeze tozo kubwa ili kupata makusanyo makubwa.

Kuhusu tozo zilizofutwa Waziri Ummy amesema kuwa kupitia bodi iliyomaliza muda wake walifanikiwa kufuta tozo zaidi ya 20 ambazo zilikua zinawaumiza wazalishaji na wafanyabiashara za madawa, vipodozi na vyakula lengo likiwa ni kumpunguzia gharama mtumiaji wa mwisho.

Ameyataja mafanikio mengine makubwa ya TMDA kuwa ni kutambulika na Shirika la Afya Duniani (WHO) kuwa ni moja ya Taasisi bora ya udhibiti dawa ambapo imefikia hatua ya umahiri namba tatu pamoja na kuwa Mamlaka ya Udhibiti ya kwanza barani Afrika kufikia hatua ya tatu ya umahiri kwenye mifumo ya udhibiti wa dawa baada ya kuhakikiwa na Shirika la Afya Duniani (WHO Maturity Level 3 Regulatory Authority); Kuweka mifumo ya utendaji kazi ambayo imefikia kiwango cha ISO 9001:2015 toka mwaka 2009; Maabara yake kuweza kufikia viwango vya ISO/IEC 17025:2015 nakupa ta ithibati ya WHO (WHO Prequalified Laboratory); Kuanzisha Ofisi za Kanda kwenye mikoa 8 kwa lengo la kusogeza huduma kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kujenga jengo la Ofisi na Maabara, Kanda ya Ziwa – Mwanza.

Hata hivyo Waziri Ummy Mwalimu ameishukuru bodi iliyomaliza muda wake ambayo ilikua chini ya Mwenyekiti Balozi Ben Moses na wajumbe wake kwa kufanikisha mafanikio makubwa yaliyofikiwa katika kipindi cha cha utendaji wao.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com