Na Zainab Nyamka - Dar es salaam
Wamekaa!!! Mchezo wa Kirafiki kati ya Yanga na KMC umemalizika kwa Yanga kukubali kipigo cha goli 3-0.
Mchezo huo umechezwa leo katika Uwanja wa Uhuru ikiwa ni mchezo wao wa pili wa kirafiki baada ya kupata ushindi wa 3-1 dhidi ya Transit Camp.
Mpira ulianza kwa kasi KMC wakitawala mchezo kwa dakika za mwanzo kabla ya Yanga kubadilisha mchezo na kuonekana kuutawala.
KMC walichukua dakika 31 kuweza kuandika goli la kwanza kupitia kwa Sadala Lipangile akipokea pasi ya Charlse Ilanfya.
Dakika ya 45 kabla ya mapumziko, KMC wanaandika goli pili kupitia kwa Ilanfya kwa pasi safi ya Emmanuel Mvuyekule.
Hadi mapumziko KMC wanatoka wakiwa mbele kwa goli 2-0 dhidi ya Yanga.
Hassan Kabunda anaiandikia KMC goli lingine akipiga faulo iliyomshinda mlinda mlango Metacha Mnata na kuiandikia KMC goli la tatu na la ushindi.
Hadi mpira unamalizika KMC walitoka kifua mbele kwa ushindi wa goli 3-0.
Mchezo unaofuata wa Yanga utakuwa ni wa Ligi Kuu dhidi ya Mwadui ambapo ni mchezo wa Kiporo utakaochezwa katika dimba la Kambarage Mkoani Shinyanga.'
Social Plugin