MKAZI wa Mbuyu Zanzibar, Daurat Salum Suleiman amehukumiwa kulipa faini ya Sh milioni tano au kutumikia kifungo cha miaka miwili jela baada ya kupatikana na hatia ya kumtusi mama yake mkubwa kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram.
Suleiman alihukumiwa kifungo hicho katika Mahakama ya Ilala jijini Dar es Salaam mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Martha Mpaze.
Hakimu Mpaze alisema upande wa mashitaka ulipeleka mahakamani hapo mashahidi sita kuthibitisha mashitaka ya udhalilishaji kwa njia ya mtandao na kwamba wameweza kuthibitisha mashitaka hayo bila kuacha shaka lolote.
Alisema baada ya kusikiliza mashahidi wa alibaini maneno aliyoandika mshitakiwa yalikuwa na lengo la kumdhalilisha mlalamikaji Shabaha Said Chondoma maarufu kwa jina la teacher licha ya kwamba Suleiman alikataa kutenda kosa hilo wakati akijitetea.
"Baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi sita na vielelezo, mahakama inakutia hatiani kwa kumdhalilisha kimtandao Chondoma hivyo, utatakiwa kulipa faini ya Sh milioni tano na akishindwa kulipa fedha hiyo atatumikia kifungo cha miaka miwili jela," alisema Hakimu Mpaze.
Social Plugin