Furaha Dominic Jacob
Furaha Dominic Jacob ameongoza kura za maoni Jimbo la Kawe, Dar es Salaam kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kupata kura 101 kati ya kura zote 475.
Mkutano huo wa kura za maoni imefanyika leo Jumanne tarehe 21 Julai 2020.
Aliyeshika nafasi ya pili ni, Angela Kiziga kura 85 na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amekuwa nafasi ya tatu kura 79 na meya wa zamani wa Manispaa ya Kinondoni, Benjamin Sitta akepata kura 61.
Mkurugenzi Mkuu wa zamani wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Francis Nanai ameibuka na kura tano huku aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Moshi Mkoa wa Kilimanjaro, Kippi Warioba amepata kura tatu.
Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vicent Mashinji yeye amejikuta akipata kura mbili.
Askofu Josephat Gwajima
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Kate Kamba amesema hizi ni kura za maoni, hakuna mshindi au aliyeshindwa na kuwaomba wagombea wasubiri michakati mingine iendelee.
CCM imesema inajipanga kupata mgombea atakayeweza kulichukua jimbo hilo ambalo kwa miaka kumi mfululizo linaongozwa na Halima Mdee wa Chadema ambaye naye tayari ameshinda kura za maoni.
Dk. Vincent Mashinji
Baada ya matokeo hayo, Dk. Mashinji ameandika katika ukurasa wake wa Twitter akisema, “nawashukuru wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM, Jimbo la Kawe kwa heshima kubwa waliyonipa kama mtia nia wa ubunge.”
“Utulivu wa kisiasa ndani na nje ya ukumbi, umenipa faraja kubwa sana na hamasa ya ushindi, katika uchaguzi ujao. Tunarejesha CCM, Kawe. Umoja wetu ni ushindi wetu!,” ameandika Dk. Mashinji