Na Mwandishi wetu Lindi
WAKATI Tanzania ikiendelea na mombolezo kufuatia kumpoteza aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamini Mkapa, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania katika Awamu ya Nne, Bernard Membe amesema Mkapa alikuwa Kiongozi wa dunia.
Membe ameyasema hayo jana mkoani Lindi, muda mchache baada ya kuahirisha Kikao cha Chama Cha ACT Wazalendo kilichokuwa kifanyike mjini humo sambamba na kukutana na viongozi mbalimbali wa Chama ngazi za kata.
Akimzungumzia marehemu Mkapa, Membe amesema, alikuwa kinara katika kusaidia bara la Afrika kuweza kutatua migogoro bila kuchoka hatua ambayo imeacha pigo kubwa.
"Kwanza nichukue nafasi hii kwa niaba ya familia na Wana-ACT Wazalendo kutoa salamu zetu za pole ole za dhati kwa kabisa katika msiba huu mzito uliotukuta..., Mzee Mkapa ambaye ni Baba yetu na Rais mstaafu alikuwa kiongozi siyo wa Tanzania tu bali alikuwa kiongozi wa dunia, amesuluhisha migogoro mingi, nimepokea salamu kutoka kwa Waziri wa Namibia akitoa salamu zake", amesema Membe.
"Tutamkumbuka kwa kuwa kiongozi ambaye alitumia wakati wake mwingi kuisaidia jamii ya Tanzania, alikuwa miongoni mwa marais wazuri wa Tanzania, kifo chake kimetuletea majonzi watu wote," ameongeza Membe.
Amesema yeye kama Mwana-diplomasia atamkumbuka, Mzee Mkapa kwa elimu yake, ushauri wake, maagizo yake na mafundisho yake juu ya diplomasia ya kweli, diplomasia ya kisiasa na diplomasia ya uchumi ambayo alikuwa anaisimamia.
"Nchi kama Msumbiji, Namibia, Afrika Kusini, Burundi, Rwanda, Kenya, Sudani na Congo Mzee Mkapa ameshiriki katika utatuzi wa migogoro mbalimbali tangu aache nafasi yake ya urais mwaka 2005.
"Nina hakika baada ya kifo hiki dunia itamkumbuka kama kiongozi mashuhuri barani Afrika na duniani kwa ujumla kwa kuweza kutatua migogoro mbalimbali iliyokuwa ikiikabili Afrika bila kuchoka kwa muda wote alipotakiwa kufanya hivyo."
Aidha, Membe ameongeza kuwa ni pigo kuona kiongozi huyo mkubwa akiondoka katika wakati ambao Tanzania inaelekea katika uchaguzi Mkuu Oktoba 28, Mwaka huu.
"Katika kipindi cha Uchaguzi kama hiki ni bahati mbaya kuona kwamba tunampoteza mtu ambaye alikuwa anahimili mambo mengi ya uchaguzi ikiwa ni pamoja na ushiriki wake na ushauri katika masula ya uchaguzi.
"Ni bahati mbaya kwamba kwa mwaka huu ambapo uchaguzi utakuwa mkubwa na mkali zaidi tumempoteza mshauri mkuu wa masuala ya uchaguzi ya kitaifa lakini Mwenyezi Mungu atatusaidia, na hakika atendelea kubaki mioyoni mwetu," amesema Membe.
Amesema Wanachama na Viongozi wa ACT Wazalendo wamelazimika kuahirisha shughuli zote za chama ili kumpa heshima kiongozi huyo ambapo watalazimika kurejea Dar es Salaam kwa ajili ya kutoa heshima za mwisho na kisha kuelekea Masasi mkoani Mtwara kwa ajili ya kushiriki mazishi.
Rais mstaafu Mkapa alifariki Julai 23, mwaka huu katika Hospitali jijini Dar es Salaam alikokuwa amelazwa akipatiwa matibabu ambapo anatarajiwa kuzikwa mkoani Mtwara jumatano Julai 29,2020 ya wiki ijayo.
Social Plugin