Aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa enzi za uhai wake
Na Said Mwishehe, Michuzi TV.
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ametangaza ratiba ya mazishi ya kifo cha mpendwa wetu Rais mstaafu Benjamin Mkapa ambaye atazikwa Julai 29 mwaka huu kijijini kwake Lupaso wilayani Masasi mkoani Mtwara na mwili wake utaagwa katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Akitangaza ratiba hiyo jana Julai 24,2020 jijini Dar es Salaam ,Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kwamba "Kama ambavyo imetangazwa kifo cha mpendwa wetu , kiongozi wetu, mzee wetu na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu mzee wetu Benjamin Mkapa ambaye ametutangulia mbele za haki.
"Mheshimiwa Rais amewasihi Watanzania kwamba katika kipindi hiki kigumu kwetu tuendelee kuwa watulivu, tuendelee kuwa wavumilivu na tuendeleee kumuombea Rais wetu mstaafu Benjamin William Mkapa kwa kutangulia mbele za haki,"amesema Waziri Mkuu.
Amefafanua kuwa "Na sasa nimewaita wanahabari kwa lengo la kuwapa ratiba nzima ya tukio hili mpaka siku ya mazishi, Rais wetu pamoja na Kamati ya mazishi Taifa imeshaandaa utaratibu wa mzima wa tukio hili, marehemu atakwenda kuzikwa kijijini kwake Lupaso wilayani Masasi mkoani Mtwara .
Lupaso ni kijiji kilicho kwenye mji wa Masasi na mazishi haya yatafanyika siku ya tarehe 29 Jumatano ya wiki ijayo, sasa kuanzia sasa tunaendelea kupokea waombolezaji pale nyumbani kwa marehemu, kwa wageni mbalimbali kumpa pole mke wa marehemu.
"Watoto wa marehemu na familia lakini tutatoa fursa kwa watanzania wote kuanzia Jumapili kwa kushughuli za kuaga ambazo zitafanyika Uwanja wa Taifa na Uwanja wa Uhuru haoa jijini Dar es Salaam.Shughuli za kuaga zitafanyika kwa siku tatu mfululizo kuanzi tarehe 26 mpaka tarehe 28 kwa maana ya kuanzia Jumapili mpaka Jumamne,"amesema Waziri Mkuu wakati anatangaza ratiba hiyo.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu amesema katika siku hiyo ya Jumapili kuanzia saa nne , Kanisa Katoliki litaongoza Misa ambapo watanzania watapata fursa ya kuanza kuaga mwili.
"Lakini Mtanzania yoyote ambaye hatapata fursa ya kuja Dar es Salaam atapata pia nafasi ya kwenda kuaga mwili baada ya hiyo Misa.Shughuli za kuaga mwili litaendelea kwa siku nzima na kuendelea na Siku ya Jumatatu ambayo nayo itatumika kuendelea kuaga.
"Na Jumanne ya Julai 28 ni siku ambayo itatumika kuaga mwili wa mpendwa wetu kitaifa ambapo viongozi mbalimbali wa kiserikali nchini, viongozi wa dini pamoja na wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam bado watarakabirishwa.Niwaombe wana Dar es Salaam wote kuja kwenye kuaga siku ya kitaifa ambapo viongozi wote watapa fursa ya kuaga siku hiyo.
"Pia tunakaribisha mtumishi yoyote siku hiyo kwasababu itakwenda mpaka saa sita mchana na baada hapo watumishi wataendelea kwenye shughuli zao na baada ya hapo kuaga kutaendelea mpaka saa nane mchana.
"Baada ya saa nane mwili utaandaliwa na kusafirishwa kwenda Lupaso Masasi mkoani Mtwara ambako Jumatano wana Lupaso, wana Masasi, ndugu na jamaa na wote watakaofika kwenye msiba huo watapata heshima na fursa ya kuaga mwili huo mpaka saa sita kamili na saa nane mchana siku hiyo ya Jumatano ndio mazishi yatafanyika,"amesema Waziri Mkuu.
Amefafanua sababu za kuwekwa muda wa saa nane ni kwamba wanalenga kuwapa nafasi wale wote ambao wanaamini wanatamani na wangependa kushiriki kwenye mazishi kusafiri hata kama watatoka jijini Dar es Salaam na wanaweza kufika kama saa nane na kisha wakazika na kurudi.
"Na wale ambao watasafiri kwa ndege watatumia viwanja vya ndege vya Mtwara na Nachingwea . Mwili wa marehemu utatua katika uwanja wa Nachingwea ambako kwenda Msasi pana umbali wa kilometa 35 ambako ni jirani zaidi ukulinganisha na Uwanja wa ndege Mtwara ambao uko umbali wa kilometa 110.
"Kwa hiyo nimeona niitamke ratiba hii ili Watanzania waweze kujua, kila mmoja aweze kupanga shughuli zake vizuri na kujipa nafasi ya kushiriki, na ratiba hii itasaidia hata mataifa ya nje ambayo yameguswa na msiba huu kuja kushiriki kwa kadiri ya ratiba tulivyoitoa.
"Tunao mabalozi ambao watatoa taarifa kwenye nchi zao na kwa kipindi hiki ambacho kuna "Tatizo la Corona katika nchi kadhaa basi kiongozi yoyote akiona anaweza kuja tutapata taarifa kupitia ubalozi wake uliopo hapa nchini na tufanya maandalizi ya kuwapokea na baadae kushiriki katika mazishi na kisha ubalozi utaangalia namna ya kuwarejesha makwao.
"Hivyo niliona niwashirikishe Watanzania kuhusu ratiba hii ambayo inaanza Jumapili kwa Watanzania kupata fursa ya kushirki kwenda kuaga lakini siku ya Jumanne kama nilivyosisitiza kwa wana wa Dar es Salaam tunaomba wajitokeze kwa wingi pale uwanjwa wa uhuru kushuhudia tena kuaga kitaifa.
"Ambapo viongozi wa Bara na Visiwani watakuwepo, shughuli hiyo itakwenda mpaka saa sita mchana na baada ya hapo mwili utakwenda monchwari kwa maandalizi na saa tisa utasafirishwa kuelekea Masasi,hiyo ndio taarifa muhimu niliyoona niwashirikishe,"amesema Waziri Mkuu.
Wakati huo huo, WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ametia saini kitabu cha maombolezo ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa kilichotokea jijini Dar es Salaam na ametoa pole kwa familia kwa niaba ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Serikali.
“Ndugu wanafamilia, kwa niaba ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli na Serikali tumepokea taarifa za msiba wa mzee wetu, kiongozi wetu Rais wa Awamu ya Tatu kwa masikitiko makubwa. Nawasihi muendelee kuwa watulivu na wavumilivu katika kipindi hiki kigumu kama alivyosema Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Magufuli.”
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa, Julai 24, 2020) nyumbani kwa marehemu Masaki, jijini Dar es Salaam. Amewasihi wanafamilia na Watanzania kwa ujumla waendelee kumuombea marehemu kwa Mwenyezi Mungu kwa sababu yote ni mapenzi yake.
Amesema kamati ya mazishi ya Serikali inaendelea na maandalizi pamoja na kuwasiliana na viongozi kutoka katika nchi marafiki ambao marehemu alifanya nao kazi ili kutoa fursa ya wao kushiriki. “Tutatoa taarifa ya ratiba ya kuaga mwili itakayofanyika Uwanja wa Taifa.”
Kufuatia kifo hicho kilichotokea usiku wa kuamkia leo, Rais Dkt. Magufuli ametangaza siku saba za maombolezo ya Kitaifa kuanzia leo Ijumaa, Julai 24, 2020 na katika kipindi chote cha maombolezo bendera zote zitapepea nusu mlingoti.
Akitangaza kifo hicho kwa Watanzania kupitia vyombo vya habari usiku wa kuamkia leo Rais Dkt. Magufuli kwa masikitiko makubwa alisema Rais wa Awamu ya Tatu, Mhe. Benjamini William Mkapa amefariki dunia hospitalini jijini Dar es Salaam ambako alikuwa akipatiwa matibabu.
Rais Dkt. Magufuli amewataka Watanzania wote wawe watulivu na wastahimilivu baada ya kupokea taarifa za kuondokewa na mpendwa wao Mhe. Benjamin William Mkapa. “Kwa masikitiko makubwa tumepata msiba mkubwa, Mzee wetu Benjamin William Mkapa, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu amefariki dunia.”
Aliongeza kuwa “ Amefariki dunia katika hospitali jijini Dar es Salaam ambako alikuwa amelazwa, niwaombe Watanzania tulipokee hili, tumepata msiba mkubwa na tuendelee kumuombea Mzee wetu Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa, ambaye ametangulia mbele za haki.”
Social Plugin