Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAMIA YA WANANCHI WAANZA KUAGA MWILI WA RAIS MSTAAFU BENJAMIN MKAPA KATIKA UWANJA WA UHURU DAR

Na Said Mwishehe,Michuzi TV
MAMIA ya wananchi wa Jiji la Dar es Salaam wameanza kujitokeza kwa wingi katika Uwanja wa Uhuru ambako shughuli za kuaga na kutoa heshima za mwisho kwa Rais Mstaafu Benjamin Mkapa zinaendelea kuanzia leo Jumapili,Jumatatu na Jumanne kabla ya mwili wake kupelekwa kijijini kwake Lupaso mkoani Mtwara kwa kumpumzisha katika nyumba yake ya milele.

Uwanjani hapo simanzi, huzuni,majonzi na kila aina ya machungu yameendelea kutawala ambako wananchi watapa fursa ya kuaga mwili wa Rais mstaafu Benjamin Mkapa. Hakika wananchi wa Jiji la Dar es Salaam wameonesha kuguswa na msiba wa kitaifa na kila mmoja amekuwa na shauku ya kutoa heshima za mwisho.

Wananchi walianza kujitokeza mapema ya leo asubuhi ya Julai 26 na kadri muda ulivyokuwa ukienda ndivyo idadi ya watu ilivyokuwa ikiongezeka.Mbali ya wananchi kujitokeza kwa wingi uwanjani hapo pia kulikuwa na viongozi wa ngazi mbalimbali waliopata fursa ya kushiriki Misa maalum iliyoandaliwa kwa ajili ya kufanya ibada kabla ya wananchi kuanza kutoa heshima zao za mwisho kwa mpendwa wetu mzee Benjamin Mkapa aliyefariki dunia juzi Julai 24 jijini Dar es Salaam.

Baada ya kumalizika kwa Misa hiyo ndipo ukawadia muda wa kuanza kuaga. Hata hivyo kwa mujibu wa ratiba shughuli za kuaga zitafanyika kwa siku tatu mfululizo na Jumanne itakuwa siku ya kuaga kitaifa ambako viongozi mbalimbali watashiriki.

Pia kutakuwa na viongozi na wawakilishi wa nchi mbalimbali barani Afrika na nchi nyingine nje ya bara hilo watashiriki siku hiyo. Serikali kwa mujibu wa Msemaji Mkuu wa Serikali Dk.Hassan Abbas ni kwamba wameendelea kupokea salamu za rambirambi kutoka kila kona ya pembe ya dunia.

Mwili wa mzee Mkapa ulipelekwa uwanjani hapo kwa gari maalum ya kijeshi iliyokuwa imeandaliwa kubeba jeneza lenye mwili wake na wakati gari hiyo ikiwa inapita kuna wananchi waliokuwa wamesimama kando ya barabara ikiwa ni kuonesha upendo wao kwa Rais wetu mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu.

Jana wakati Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Abubakar Kunenge anazungumzia ratiba ya shughuli za kuaga mwili, ametumia nafasi hiyo kuomba wananchi kujitokeza kwa wingi kutoa heshima zao za mwisho..

Hata hivyo baada ya shughuli za kuaga zitakapokamilika ratiba iliyokuwa imetolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ilikuwa inaeleza mwili wa mzee Mkapa utapumzishwa kwenye nyumba yake ya milele Jumatano ya wiki ijayo saa nane mchana na sababu za kuwekwa kwa muda huo ni kutoa fursa kwa wanaosafiri kutoka mengine wakiwemo wa Dar es Salaam kuwahi mazishi na kisha kurudi makwao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com