Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SABABU YA KIFO CHA RAIS MSTAAFU BENJAMIN MKAPA YATAJWA


Na Said Mwishehe,Michuzi TV

WATANZANIA wameelezwa kwamba sababu za kifo cha Rais Mstaafu Benjamin Mkapa ni mshutuko wa moyo ambao aliupata alipokuwa anasikiliza taarifa ya habari Julai 23 mwaka huu.

Imefafanuliwa alipokuwa akisiliza taarifa ya habari alipotaka kuinuka kutoka eneo alilokuwa amekaa lakini alishindwa na kisha akawa amekaa akiwa ameinamisha kichwa chake na baada ya vipimo ilithibitika mzee wetu amefariki dunia.

Hayo yameelezwa leo Julai 26,2020 jijini Dar es Salaam wakati wa Misa maalum ya kumuombea mzee wetu Benjamin Mkapa iliyofanyika Uwanja wa Uhuru ambako shughuli za kuaga mwili wake zinafanyika kuanzia leo,kesho na keshokutwa.

Msemaji wa familia ya Mzee Mkapa William Urio amefafanua kwamba kumekuwepo na maneno mengi yanayoendelea tangu mzee wetu alipofariki dunia lakini ni vema ikafahamika kilishosababisha kifo chake ni mshtuko wa moyo.

" Kabla ya kupatwa na mshtuko wa moyo mzee Mkapa alikuwa hajisikii vizuri,hivyo alipelekwa Hospitalini kwa ajili ya vipimo vilivyoonesha kuwa na Malaria, akaanza matibabu siku ile ya Jumatano na mchana akawa anaendelea vizuri tu.

" Siku hiyo pia alipata nafasi ya kuangalia  mchakato wa kura za maoni za wabunge ambazo zilikuwa zinarushwa mubashara ,baadae akawa anasikiliza taarifa ya habari na alipotaka kuinuka akashindwa,hivyo akakaa na kuinamisha kichwa chake.

"Kutokana na hali hiyo ikabidi vifanyike vipimo ambavyo vilithibitisha ameshafariki dunia,"amesema Urio ambaye ndio msemaji wa familia huku akiomba kwa Watanzania kuelewa kwamba huo ndio ukweli na vema ukaheshimiwa na kila mmoja wetu.

Pia imetumia nafasi hiyo kuishukuru Serikali, viongozi wa dini, viongozi wa vyama, waandishi wa habari na wananchi mbalimbali kwa kuendelea kuwa nao bega kwa bega kwa kuwafariji katika kipindi hiki kigumu wanachopitia kwa kumpoteza mpendwa wao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com