Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga akizungumza na Wakulima, Waoneshaji na wadau wengine wa Kilimo kabla ya kuzindua rasmi maonesho hayo ya Kilimo Biashara yaliyofanyika kwenye viwanja vya Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Selian cha Jijini Arusha.
Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga akikabidhi majembe matano ya kukokotwa na ng'ombe yaliyotokewa na Kituo cha Utafiti cha Selian kwa kikundi cha Wakulima kinachofanya kazi karibu sana na kituo hicho. ( kwenye picha ni baadhi ya viongozi wa kikundi hicho.)
Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo Cha Selian cha Jijini Arusha Dkt. Joseph Ndunguru akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufunguliwa rasmi kwa maonesho hayo kituoni hapo.
Bango la maonesho hayo.
Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga akikata keki iliyotengenezwa kwa kutumia unga wa maharage ambayo lengo lake ilikuwa kuonesha matumizi mbalimbali ya maharage katika jamii.
Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga pamoja na wananchi na viongozi wengine waliotembelea vipando vya mazao mbalimbali vilivyopandwa kuonesha teknolojia mbalimbali za Kilimo.
Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, akitembelea mabanda katika maonesho hayo.
Na Calvin Gwabara, Arusha
WAZIRI wa Kilimo Japhet Hasunga amesema Wakulima na Wizara yake imempoteza Kiongozi ambaye si tu kwamba alisisitiza Watanzania kutumia nguvu zao kama mtaji katika kufanya kazi bali aliyehakikisha kilimo kinatoa mchango mkubwa katika maendeleo yao na Taifa.
Akizungumza kwenye Maonesho ya Kilimo Biashara yaliyofanyika kwenye Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Selian cha Jijini Arusha Hasunga alisema kuna mambo mengi sana ambayo tunajivunia leo kwenye Kilimo yametoka na mchango Mkubwa wa Rais wa Awamu ya Tatu Marehemu Mhe. Benjamin William Mkapa.
Akizungumzia baadhi ya mambo hayo alisema ni msimamo wake thabiti katika kuhakikisha wataalamu wa kilimo kwa ngazi zote wanatoka maofisini na kwenda kutoa elimu stahiki kwa wakulima na wafugaji ili kilimo kinachotegemewa na zaidi ya asilimia 75 ya watanzania kitoe mchango unaostahili.
“Aliposema mtaji wa masikini ni nguvu zake mwenyewe alisisitiza watu kutumia nguvu zao kama mtaji katika uzalishaji mali kwa kufanya kazi mbalimbali hasa za kilimo ili kutokomeza njaa na umasikini kwenye kaya.” alisema Hasunga.
Waziri huyo wa kilimo pia akibainisha kuwa uanzishwaji wa TASAF ilikuwa ni moja ya jitihada za kusaidia kaya masikini ambazo nyingi zipo vijijini zinajishughulisha na kilimo huku akipambana na rushwa kwa kuanisha Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) ili masikini wapate haki kwenye ofisi za serikali na kwenye maeneo mengine wanapokwenda kutafuta huduma.
“ Niwatakie watanzania hasa wakulima na wataalmu wa kilimo kumuenzi kwa vitendo Marehemu Benjamin Mkapa kwa yale yote ambayo aliyaanzisha na kuyasisitiza ili kuwakomboa watanzania wanyonge na wale wenye kipato cha chini” alisisitiza Hasunga.
Waziri huyo wa kilimo ameipongeza Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania TARI na Kituo cha Utafiti cha Selian cha Jijini Arusha kwa kuandaa maonesho hayo ya Kilimo Biashara kwa lengo la kuwezesha wakulima kujionea na kujifunza teknolojia mbalimbali za kisasa za kilimo ili ziwaisaidie kuboresha kilimo chao na kuongeza tija.
Alisema kilimo cha kizamani na cha kutumia mbegu za asili hakina tija kwa mtazamo wa kibiashara na badala yake watumie mbegu zilizoboreshwa ili wazalishe zaidi na kupata ziada lakini serikali haizuii wakulima kulima mbegu za asili lakini tafiti zinaonesha mbegu za asili hazina tija sana kutoka na uwezo wake wa kushindwa kuhimili Magonjwa, Wadudu na mabadiliko ya tabia nchi.
Awali akieleza malengo ya maonesho hayo Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Selian cha Jijini Arusha ambao ndio walioandaa maonesho hayo Dkt. Joseph Ndunguru alisema ni kuwaonesha wadau wote wa kilimo teknolojia, mbinu na aina mbalimbali za mbegu ambazo wamezalisha ili Wakulima wazione na kuchagua zinazowafaa kwenye maeneo yao.
Alisema kituo hicho ambacho kina dhamana kwenye utafiti wa maharage nimezalisha mbegu mbalimbali za maharage ambayo yana sifa mbalimbali ambazo ni kuvumilia magonjwa, zenye viinilishe mbalimbali hasa madini ya chuma, zinazoendana na mabadiliko ya tabia nchi pamoja na zinazofaaa kwa usindikaji kutimiza ndoto ya Tanzania ya Viwanda.
Dkt. Ndunguru alisema pamoja na kuonesha kazi zinazofanywa na kituo hicho pia wametoa nafasi kwa wadau wengine wa kilimo hasa makampuni ya mbegu na pembejeo zingine kuonesha bidhaa wanazozalisha ili wananchi wapate uwanja moana zaidi wa kuchagua kulingana na mahitaji yao ya Kilimo kwenye maeneo yao.
Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dkt. Geofrey Mkamilo alisema Taasisi hiyo ina vituo 17 nchi nzima ambavyo vinafanga kazi kubwa ya kuzalisha teknolojia mbalimbali kulingana na mahitaji ya kanda husika za kilimo na kwamba kazi kubwa iliyo mbele yao ni kuhakikisha matokeo hayo mazuri ya Utafiti kwenye kila kituo ya wafikia wadau wote wa Kilimo ili wazitumie na kuongeza uzalishaji.
“ Niwaatamkie leo rasmi waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali nchini nyinyi ni sehemu ya TARI na naomba wakurugenzi wote wa vituo kokote nchini kufanya kazi na waandishi wa habari ili wasaidie kufikisha matunda ya tafiti zetu kwa jamii kwa upana wake maana hatuwezi kufika kila mahali kama ambavyo vyombo vya habari vinafika” alisisitiza Dkt. Mkamilo.
Aidha, Mkurugenzi huyo Mkuu wa TARI alisema kuwa hivi sasa wameanzisha utaratibu mzuri ambao vituo vyote vya utafiti vitakuwa vinashamba la maonesho kwenye vituo vyao kuonesha teknolojia mbalimbali wanazozalisha kwa Mwaka mzima ili wananchi wakaone na kujifunza badala ya kutegemea wakati wa maonesho ya nanenane pekee ambayo hufanyika siku nanenane tu kwa mwaka.
Nao baadhi ya wakulima walioshiriki kwenye maonesho hayo ya Kilimo Biashara kwenye kituo cha Utafiti cha Selian Jijini Arusha wamemuomba waziri wa kilimo kusaidia somo ka kilimo kuanza kufundishwa kuanzia shule za msingi ili wale wanaoshindwa kuendelea na elimu ya juu washiriki kwenye kilimo kwa kulima kisasa.
Katika kutambua mchango wa vikundi vya wakulima Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Selian Dkt. Joseph Nduguru alijibu ombi ka Kikundi cha wakulima kilichotembelea maonesho hayo ombi lao la kupatiwa majembe ya kukokota na ng’ombe matano ambayo yalikabidhiwa na Mhe. waziri wa kilimo huku mdau mwingine Mero Agro akiongezea majembe mengine mawili na hivyo kupata majembe 7.
Social Plugin