Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TIP YATUMIA WANAWAKE MASHUHURI KUTOKOMEZA UKATILI WA WATOTO


Meneja Mradi wa TIP  wilaya ya Sengerema Bi. Asina Shenduli 

Na Ellukagha Kyusa - Buchosa
Umoja wa Taasisi nne za dini nchini (TIP) ikishirikiana na wadau mbalimbali imewatumia wanawake wenye ushawishi kutokomeza ukatili wa kingono kwa watoto kupitia mradi wa Boresha unaotekelezwa kwenye  halmashauri ya Buchosa iliyopo katika wilaya ya Sengerema Mkoa wa Mwanza.

Meneja Mradi wa TIP  Wilaya ya Sengerema Bi. Asina Shenduli ameeleza kuwa wanawake wamekuwa mstari wa mbele na watu wa  karibu zaidi katika malezi ya watoto hivyo inakuwa rahisi kuwatumia wanawake hao katika kusambaza elimu juu ya unyanyasaji wa kingono kwa watoto pamoja na kushirikiana viongozi wa dini katika kusambaza elimu hiyo.

Sheduli aliongeza kuwa,  wanawake hao wenye ushawishi wana nafasi ya kuunda vikundi vya kuhamasisha jamii ndani ya jamii ili kutoa elimu ya kupiga vita ukatili wa kingono kwa watoto sanjali na umuhimu wa fomu namba tatu kwa jamii ili kulinda haki za watoto.

Kwa upande wao,wananchi akiwemo Doricas Lenatus na Jofrey Zacharia wamesema wanahitaji elimu ya kutosha juu ya umuhimu wa fomu namba  tatu ya polisi (PF3)  kutokana na kutofahamu chochote kuhusiana na fomu hiyo  pamoja na kutojua umuhimu wa  ufatiliaji wa fomu hiyo na faida zake katika kukamilisha ushahidi wa mashtaka katika ngazi ya mahakama.

Afisa Ustawi katika Halmashauri ya Buchosa  Rehema Katany ameeleza kuwa kumekuwa na changamoto ya kutokuwa na ushirikiano wa kutosha baina ya wananchi pamoja na uongozi dhidi ya kesi za unyanyasaji wa kingono kwa watoto na asilimia kubwa ya wananchi wamekuwa wakimaliza kesi hizo kwa mazungumzo ya kifamilia au kulipana fedha kitu ambacho si sahihi katika kuitafuta haki ya mtoto aliyefanyiwa ukatili wa kingono.

 TIP kupitia Mradi wa Boresha  inendelea kusambaza elimu ya kutosha kwa wakazi wa halmashauri hiyo kutasaidia kupunguza unyanyasaji wa kingono kwa watoto na sheria stakihi dhidi ya mtuhumiwa zikichukuliwa itakuwa ni fundisho kwa wanao tenda vitendo vya ukatili kwa watoto.

Taasisi ya TIP inajumuisha taasisi nne za kidini zikiwemo,Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA),Umoja wa makanisa ya kikristo Tanzania (CCT),Baraza la maaskofu (TEC), pamoja na Ofisi ya Mufti Zanzibar (MoZ)

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com