ANNA HENGA ATEULIWA KUWA MJUMBE WA BODI YA WAKURUGENZI YA BARAZA LA ASASI ZA KIRAIA AFRIKA


Bi. Anna Henga
Freetown, Sierra Leone, Julai 13, 2020
Bodi ya Wakurugenzi ya Baraza la Asasi za Kiraia Barani Afrika (African NGO Council) imemteua Bi. Anna Henga (Wakili) kuwa mjumbe mpya wa bodi hiyo. Wakili Anna Henga, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), atakuwa mjumbe wa bodi ya Baraza hilo kwa muda wa miaka miwili, kuanzia Julai 2020.

Katika barua ya uteuzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Asasi za Kiraia Barani Afrika, Rebecca Paulson, amempongeza Anna Henga kwa uteuzi huo na kumkaribisha katika bodi ya wakurugenzi ya Baraza hilo.

“Nina furaha sana kukukaribisha kuitumikia Bodi ya Wakurugenzi ya Baraza la Asasi za Kiraia Barani Afrika. Katika mkutano wa Kamati ya Uteuzi ya Bodi hii, uliofanyika Julai 1, 2020, wajumbe waliafiki kukuteua kuwa mjumbe mpya ya Bodi ya Wakurugenzi. Hivyo, kwa barua hii umeteuliwa rasmi kuongoza na kutoa uelekeo wa kimkakati kwa Baraza la Asasi za Kiraia Barani Afrika (African NGO Council) kwa kipinfdi cha miaka miwili ijayo kuanzia Julai 2020”,amesema Rebecca katika barua ya uteuzi.

Kwa upande wake, Anna Henga ameonesha furaha yake kwa kupata nafasi hiyo adhimu huku akiahidi kutoa mchango wake katika kufikia malengo ya Baraza hilo.

“Nimefurahishwa sana kupata wito huu wa kuteuliwa. Ni heshima kubwa kupata nafasi hii adhimu ya kulitumikia bara la Afrika kupitia Baraza la Asasi za Kiraia (African NGO) Council). Baraza hili ni mwamvuli wa asasi za kiraia kwa baraza la Afrika na ninatazamia kutoa mchango wangu katika kufanikisha malengo ya Baraza hili”,amesema Henga.

Bodi ya Wakurugenzi ya Baraza la Asasi za Kiraia Afrika inaundwa na wajumbe sita, ambao hutumikia bodi hiyo kwa kipindi cha miaka miwili. Moja ya kazi kuu ya bodi hiyo ni kuongoza Baraza la Asasi za Kiraia Afrika katika kuweka mikakati na sera za zitakazowezesha kufikia malengo ya Baraza hilo.

Kuhusu Baraza la Asasi za Kiraia Afrika (African NGO Council)

Baraza la Asasi za Kiraia Afrika (African NGO Council) ni taasisi ya kikanda inayoundwa na mashirika ya kimataifa, kikanda na kitaifa yanayofanya kazi kwa lengo la kufikia uendelevu wa mazingira, kudumisha amani, kulinda haki za binadamu, utawala bora na maendeleo endelevu ya binadamu katika bara la Afrika.

Kwa taarifa zaidi kuhusu Baraza la Asasi za Kiraia Afrika tembelea https://africanngocouncil.org.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post