BASI LA KYELA EXPRESS LAPATA AJALI


JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia Dereva wa Basi la Kampuni ya Kyela Express DENIS LAMECK [48] aliyekuwa akiendesha Gari yenye namba za usajili T. 756 DEF Scania Basi baada ya kusababisha ajali iliyopelekea kifo cha mtu mmoja aitwaye AIDA IPONJA [42] Mkazi wa Masukulu.


Ajali hiyo imetokea mnamo tarehe 16.07.2020 majira ya saa 22:20 Usiku huko Kijiji cha Kyimbila kilichopo Kata ya Mpuguso, Tarafa ya Pakati, Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya katika barabara ya Tukuyu – Kyela ambapo Gari hilo Basi la Abiria Mali ya Kampuni ya Kyela Express lilikuwa likitokea Dar es Salaam kuelekea Kyela iliacha njia na kupinduka na kusababisha kifo kwa abiria mmoja.

Aidha katika ajali hiyo abiria wanne walijeruhiwa ambao ni:-
  1.     SALOME SHIMITA [43] Mkazi wa Kyela.

  2.     SABINA JOSEPH [19] Mkazi wa Kyela.

  3.     TALAMPE KANYENYE [41] Mkazi wa Kyela.

  4.     PASCHAL MERIMERI [36] Mkazi wa Jijini Mbeya.
Majeruhi wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Rungwe Makandana. Chanzo cha ajali ni mwendo kasi katika eneo lenye mkungu na mvua. Mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitalini hapo. Upelelezi unaendelea.

KUPATIKANA NA POMBE HARAMU YA MOSHI [GONGO].
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia GWANTWA ELIAS [30] Mkazi wa Itunge Wilayani Kyela akiwa na pombe haramu ya moshi (gongo) ujazo wa lita 100.

Mtuhumiwa amekamatwa mnamo tarehe 16.07.2020 majira ya saa 09:30 Asubuhi huko Kijiji na Kata ya Itunge, Tarafa ya Unyakyusa, Wilaya ya Kyela, Mkoa wa Mbeya. Mtuhumiwa ni muuzaji wa Pombe hiyo na atafikishwa mahakamani leo tarehe 17.07.2020.

 Imetolewa na;
[ULRICH O. MATEI -SACP]
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post