Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BILIONEA LAIZER AWA KIVUTIO KATIKA MAONYESHO YA BIASHARA YA 44 YA KITAIFA SABASABA JIJINI DAR


Bilionea wa Madini ambaye ni mchimbaji mdogo wa Madini Merelani mkoani Manyara, Saniniu Laizer jana alikuwa kivutio katika Maonyesho ya Biashara ya 44 ya Kitaifa Sabasaba baada ya kufikia katika viwanja hivyo na kumtembelea mabanda mbalimbali huku akinunua bidhaa kadhaa.


Bilionea huyo alifika katika viwanja hivyo saa 4 asubuhi akiwa kwenye gari aina ya Land Cruiser akiwa ameambatana na watendaji wa Tume ya Madini , Viwanda na Biashara, Chama cha Msalaba Mwekundu, skauti pamoja na wananchi mbalimbali waliohudhuria katika Maonyesho hayo.

Akizungumza mara baada ya kufanyia ziara fupi ya kumtembelea mabanda mbalimbali katika Banda la Tume ya Madini, Katibu Mtendaji wa Tume ya hiyo, Profesa Shukrani Manya alisema, upatikanaji wa madini ya Laizer ni matokeo ya ujenzi wa ukuta wa Mirerani na uwepo wa miundombinu wezeshi ya vituo vya madini katika mikoa mbalimbali.

Alisema awali wachimbaji wadogo walikuwa wakidhurumiwa madini yao kwa sababu ya kukosekana ulinzi na masoko ya uhakika lakini kwa sasa Serikali imejiimarisha na kila mchimbaji ananufaika na anachokipata.

Alisema anashukuru upatikanaji wa madini yenye uzito wa gramu 14.13 ya Laizer yenye thamani ya Sh bilioni 7.7 yamekuja muda muafaka kukiwa na ulinzi na ndio maana ameweza kunufaika nayo. 

Manya alisema katika miaka michache ya uwapo wa tume wamefanikiwa kuwarasimisha wachimbaji wadogo na kuwagawia maeneo hayo ambayo yamesaidia kuleta matokeo mazuri tofauti na miaka ya nyuma ambapo mengi yalikuwa yakifanyika tafiti na kuacha.

Kwa upande wake, Laizer aliishukuru serikali kwa kujenga ukuta huo kwa sababu umesaidia kupata thamani halisi ya madini yake aliyoyapata.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com