Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amekagua miradi ya elimu inayotekelezwa katika Halmashauri ya Kasulu mkoani Kigoma yenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 13.
Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa Chuo cha Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi Kasulu, Chuo cha Ualimu Kabanga na jengo la Utawala la shule ya Sekondari Grand.
Akizungumzia maendeleo ya ujenzi wa Chuo cha Ualimu Kabanga mara baada ya kukagua, Waziri Ndalichako amesema chuo hicho kinajengewa upya miundombinu yote baada ya ile ya awali kuchakaa sana na kushindwa kukarabatiwa.
Ameongeza kuwa ujenzi wa miundombinu ya chuo hicho unagharimu zaidi ya bilioni 10, na kuwa utakapokamilika utabadili taswira ya mji huo kwa kuwa majengo yanayojengwa ni ya kisasa na imara ambayo yatadumu kwa muda mrefu.
Akizungumzia mradi wa ujenzi wa jengo jipya la utawala na utengenezaji wa mfumo wa maji katika shule ya sekondari ya Grand, Profesa Ndalichako amesema umegharimu zaidi ya Shilingi milioni 534 na kwamba utakapokamilika utaongeza morali ya walimu kufundisha na kusaidia wanafunzi waliopo katika shule hiyo.
Mradi mwingine uliotembelewa na Waziri wa Elimu ni ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha wilaya ya Kasulu ambao upo katika hatua za mwisho ambao umegharimu zaidi ya Shilingi bilioni 2.97. Jumla ya majengo 15 yatajengwa na kitachukua wanafunzi 320 watakaokuwa wakilala chuoni hapo.
Waziri Ndalicahko amewataka wananchi wa wilaya ya Kasulu na mkoa wa Kigoma kwa ujumla kutumia fursa ya kuwepo kwa vyuo mbalimbali katika Halmashauri hiyo kujipatia maarifa na ujuzi utakaowawezesha kuajiriwa ama kujiajiri ili kujiletea maendeleo binafsi na ya mkoa wa Kigoma.
Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Simon Anange ameishukuru Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa namna ilivyojikita katika kupanua wigo wa elimu. Amesema kuwa katika wilaya yake kuna maeneo ambayo ni ya wafugaji na watoto hawakuwa wakienda shule lakini kwa sasa zimejengwa shule shikizi katika maeneo hayo ya mbali hivyo kuwezesha watoto kusoma na kuleta matokeo chanya.
Kanali Anange amesema baada ya Serikali kutekeleza Sera ya Elimu bila ada kumekuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi, hivyo kupelekea Serikali kupanua miundombinu katika ngazi zote za elimu ili kuwezesha fursa za masomo kwa wanafunzi ikiwemo na kuongeza walimu.
Aliongeza kuwa ujenzi wa miundombinu mbalimbali katika sekta ya elimu itawezesha vijana wa Kitanzania kupata elimu katika mazingira bora.
Naye Mratibu wa Mradi wa Uendelezaji wa Elimu ya Ualimu (TESP), Ignas Chonya amesema ujenzi wa miundombinu katika Chuo cha Ualimu Kabanga awamu ya kwanza unatarajiwa kukamilika Oktoba 2020 na chuo kitakuwa na uwezo wa kuchukua wanachuo 400 kwa wakati mmoja na kwamba chuo kinatarajiwa kuanza mafunzo mwaka huu.