Katibu wa Siasa na Uenezi CCM wilaya ya Shinyanga Mjini, Saidi Ahmedi Bwanga akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo Alhamis Julai 9,2020 kuhusu kusimamishwa uongozi Viongozi 12 wa UWT/CCM kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya rushwa. Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Katibu wa Siasa na Uenezi CCM wilaya ya Shinyanga Mjini, Saidi Ahmedi Bwanga akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo Alhamis Julai 9,2020 kuhusu kusimamishwa uongozi Viongozi 12 wa UWT kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Shinyanga Mjini kimewasimamisha uongozi Viongozi 12 wa CCM kwa tuhuma ya kujihusisha na vitendo vya rushwa kata ya Ngokolo Manispaa ya Shinyanga.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo Alhamis Julai 9,2020, Katibu wa Siasa na Uenezi CCM wilaya ya Shinyanga Mjini, Saidi Ahmedi Bwanga amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya kikao cha kamati ya siasa ya wilaya ya Shinyanga Mjini kilichoketi Julai 8,2020 kutoa mapendekezo na maazimio mbalimbali.
“Chama Cha Mapinduzi kimepokea taarifa mbalimbali kutoka vyombo vya dola ambazo zinatusikitisha za baadhi ya viongozi wetu wa Chama wamekiuka sheria na taratibu zetu za chama tulizojiwekea kwa kujihusisha na masuala ya rushwa. CCM imechukua hatua kali ili iwe fundisho kwa wale wengine ambao hawataki kubadilika”,ameeleza Bwanga.
“Katika kikao chetu cha kamati ya siasa ya wilaya ya Shinyanga Mjini kilichoketi Julai 8,2020 kilitoa mapendekezo na kuazimia mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwasimamisha uongozi/nyadhifa zao zote wale wote waliohusishwa na vitendo vya rushwa katika kata ya Ngokolo,waliokamatwa na TAKUKURU mpaka pale tutakapopata taarifa ya uchunguzi kamili kutoka vyombo vya dola itakayoeleza kuwa hawana makosa na baadae kitajua nini cha kufanya”,amefafanua Bwanga.
Amewataja viongozi wa UWT/ CCM waliosimamishwa uongozi kuwa ni Hulda Malsaba (Mwenyekiti wa UWT Kata ya Ngokolo), Pendo Mhapa (Katibu wa UWT Kata ya Ngokolo), Zulfa Hassan (Mwenezi kata ya Ngokolo), Jackline Isaro (Mjumbe wa kamati ya utekelezaji ya UWT wilaya ya Shinyanga Mjini) na Asha Mwandu (Mjumbe wa Mkutano Mkuu CCM taifa na Mjumbe wa kamati ya utekelezaji Wazazi mkoa wa Shinyanga).
Wengine ni Moshi Ndugulile (Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji UWT wilaya ya Shinyanga Mjini), Elizabeth Hange (Katibu wa UWT tawi la Ngokolo), Tabu Shaban (Katibu UWT tawi la Ngokolo), Tabu Said (Mwenyekiti tawi la Majengo Mapya),Happy Chikala (Katibu UWT tawi la Mwadui),Elizabeth Buzwizwi (Mwenyekiti UWT tawi la Majengo Mapya) na Elizabeth Benjamini (Mwenyekiti UWT tawi la Mwadui).
Julai 1,2020 Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Shinyanga ilitoa taarifa kwa vyombo ya habari kuhusu kumshikilia Mjumbe wa CCM Mkutano Mkuu Taifa CCM, Asha Mwandu Makwaiya Mkazi wa Majengo Mapya Mjini Shinyanga Juni 28,2020 kwa kosa la kutoa rushwa kwa wajumbe wa Jumuiya ya Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT).
TAKUKURU ilieleza kumkamata Bi. Asha Mwandu Makwaiya ambaye ni mkazi wa Majengo Mapya Shinyanga Mjini na Mjumbe wa CCM Mkutano Mkuu Taifa akiwa nyumbani kwa Elizabeth Donald Itete ‘Mama Buzwizwi’ ambaye ni Katibu wa UWT tawi la Mshikamano pamoja na wajumbe wengine 10 ambao ni viongozi wa UWT kata ya Ngokolo.
“Bi. Aisha Mwandu Makwaiya alitaka kugawa mashuka 10, kitenge kimoja, ndala 11 kwa wajumbe 11 wa umoja wa Jumuiya ya Wanawake CCM (UWT) kata ya Ngokolo kama kishawishi cha yeye kuchaguliwa au kuchaguliwa kwa aliyemtuma”,alisema Mkuu huyo wa TAKUKURU.
Social Plugin