Mkuu wa MKoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akifunga mafunzo maalum ya siku sita kwa wadau zaidi ya 300 kutoka katika mikoa mbalimbali nchini yaliyokuwa yameandaliwa na Baraza la Taifa la watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI (NACOPHA) kupitia “Mradi wa Hebu Tuyajenge” unaotekelezwa katika kipindi cha miaka mitano 2019-2024, unaofadhiliwa na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) katika mikoa 22 Tanzania Bara. kushoto Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Rahabu Mwagisa, Kulia Mkurugenzi wa Utatifi wa NACOPHA Pantaleo Shoki
Na John Mapepele
Mkuu wa
Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi
amempongeza Rais Magufuli kwa kuvunja rekodi ya
maendeleo kabla ya mwaka 2025 na kuifanya Tanzania kuingia kwenye nchi
za uchumi wa kati duniani Julai Mosi mwaka huu.
Huku akiwahimiza watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI nchini kufanya kazi kwa bidii bila kuwa na hofu sambamba na kumtanguliza Mungu na kutumia fursa za
mikopo inayotolewa na Serikali ya Awamu ya Tano ili ku kuinua hali za maisha na kuongeza pato la
taifa kwa ujumla
Dkt. Nchimbi ameyasema hayo leo katika Mji Mdogo wa Manyoni mkoani Singida alipokuwa akifunga mafunzo maalum ya siku sita kwa wadau zaidi ya mia 3 kutoka
katika mikoa mbalimbali nchini
yaliyokuwa yameandaliwa na Baraza la Taifa la watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI (NACOPHA) kupitia “Mradi wa Hebu Tuyajenge”.
Mradi huo unaotekelezwa katika kipindi cha miaka mitano
2019-2024,unaofadhiliwa na Shirika la Marekani la
Maendeleo ya Kimataifa (USAID) katika mikoa 22 Tanzania Bara.
Amesema kwa sasa Serikali ya Awamu ya Tano imepiga hatua kubwa ya kupiga
vita unyanyapaa dhidi ya watu wanaishi na virusi vya UKIMWI na kwamba watu wote
wana haki na fursa sawa mbele ya
Serikali yao hivyo hakuna sababu ya wao
kuendelea kujinyanyapaa wenyewe na badala yake wawe walimu wa kuwaelimisha
wengine kwenda kupima na kutambua hali zao
na kuendelea kuchapa kazi ili kuinua uchumi wan chi yetu.
“Kubwa ndugu zangu hapa ni
kumtanguliza Mungu mbele, kutoa
hofu na kuachana na mambo yote ambayo yanapelekea kudhoofu kwa afya zetu kama vile unywaji wa
pombe hata kama wake zetu wanapika kwa ajili ya biashara na badala yake tutumie
juisi lishe za matunda ya asili kama vile
Sasati, Ubuyu na Ukwaju” amesisitiza Dkt. Nchimbi
Umewaelekeza Wataalam wa
Maendeleo ya Jamii wa Mkoa wa Singida kuangalia namna ya kuja na mikakati madhubuti ya kiuendelevu
ya kuwakopesha wanaoishi na UKIMWI ili
kuwaletea maendeleo huku akisisitiza kuwa
Mkoa wake utaendelea kutekeleza mikakati iliyojiwekea ya kuinua
maisha ya wanainchi wake ikiwa ni pamoja
na mkakati wa kuwavusha salama mama na mtoto.
Aidha ameweka
msimamo wake wa kutokuonesha
nia yeyote ya kuomba ridhaa ya kugombea Ubunge katika uchaguzi wa mwaka huu
huku akiwaonya watu ambao wamekuwa wakianza kudanganya kuwa atagombea ambapo
alisisitiza kuwa nafasi
hiyo ya ukuu wa Mkoa aliyopewa na Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli ni ya
heshima kubwa.
“Naomba niliseme hili, na tayari
nimeshalisema mara kadhaa hata hivi
karibuni nilipokuwa nyumbani
kwangu, kijijini Matufa, Babati Manyara nilipo hudhuria mazishi ya mtoto wa Kaka
yangu aliyefariki
kwa ajali ya Pikipiki kwamba nilikwenda kuungana na familia yangu katika msiba wa kijana
wetu na si vinginevyo. Ninaridhika sana na nafasi hii niliyo nayo ya ukuu wa
Mkoa" alisema Dkt. Nchimbi huku akishangiliwa na umati wa wadau wa mafunzo hayo
Baadhi ya
waombolezaji wamesikika kupongeza msimamo wa kiongozi huyo, huku wakisema kuwa Msimamo huo unapaswa kuigwa na viongozi
wengine kwa kuwa umejikita katika
kuwaletea maendeleo wananchi badala ya kuwa na tamaa za madaraka.
“Binafsi nampongeza sana Mama Nchimbi
kwani kwa muda wote amekuwa aking’ang’ana na kuwaunganisha watu wote
bila kujali dini wala rangi kwa, hata sisi leo ametutia moyo sana kiasi
kwamba baada ya kutoka hapa tumekuwa na
nguvu mpya ya kuchapa kazi na
kushirikiana na Serikali yetu ya
kujiletea maendeleo Zaidi ili tutoke katika nchi za uchumi wa kati na kwenda
katika nchi tajiri duniani na tuna imani kubwa chini ya Rais wetu Magufuli
tutafika” amesema Amina Huredi ambaye ni
Mshiriki wa mafunzo hayo kutoka Singida
Mkurugenzi wa Utatifi wa NACOPHA Pantaleo Shoki amemshukuru Mkuu wa Mkoa na kumhakikishia
kuwa wataendelea kushikiana na Serikali
ili kuhakikisha kuwa malengo ya Mradi huo yanatimia kama yalivyopangwa.
Shoki
amesema Mradi unalenga kufikia
Mkakati wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na UKIMWI(UNAIDS) wa
95-95-95 yaani asilimia 95 ya watu wote
wanaoishi na maambukizi ya VVU wawe wamepima na kugundua afya zao,asilimia 95
ya watu wote waliopimwa na kukutwa na maambukizi wawe wameanza tiba na asilimia
95 walio kwenye tiba wawe wamefubaza virusi hivyo ifikapo 2030