Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe pamoja na makada wengine watatu wamejiengua katika kinyang’anyiro cha kuomba kuteuliwa na chama hicho kugombea urais wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020.
Wanachama hao walikuwa miongoni mwa 11 waliotia nia kuwania urais ndani ya chama hicho lakini hawakujitokeza kuchukua fomu pindi shughuli ya uchukuaji na urejeshaji ilipoanza tarehe 4 hadi 19 Julai 2020.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Chama cha Chadema, Rebby Munisi amesema watia nia waliochukua na kurejesha fomu ni Wakili Simba Neo, Aliyekuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita, Mchungaji Leonard Manyama, Dk.Maryrose Majinge, Wakili Gaspar Mwanalyela, Lazaro Nyalandu na makamu mwenyekiti wa chama hicho Bara, Tundu Lissu.
Miongoni mwa watia nia ambao hawakuchukua fomu za urais ni pamoja na Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Nalo Opiyo na Msafiri Shabani.