Katibu Mtendaji wa MCT, Bw. Kajubi Mukajanga
Na Mwandishi wetu
Baraza
la Habari Tanzania (MCT), limesema kuwa waandishi waliojitokeza kuchukua fomu
za kugombea nafasi mbali mbali za kisiasa ni haki yao ya msingi kama walivyo raia
wengine hapa nchini, lakini wanapaswa kuondoka katika uandishi wa habari.
Katibu
Mtendaji wa MCT, Bw. Kajubi Mukajanga ameyasema hayo wakati wa mahojiano na waandishi
wa habari katika ofisi za Baraza hilo leo (Julai 22, 2020), na kuongeza kwamba
mwandishi wa habari kama sehemu ya jamii ana haki ya kuwa mpiga kura na pia ana haki ya kuwa
mpigiwa kura.
“Hilo
halina mjadala inatakiwa aondoke kwa sababu hakuna namna ambayo tutaendelea kumwamini
wakati yeye amevaa shati la kijani, au la zambarau, au la blue na anapiga sera
za chama, haiwezekani akaendelea kuwa ndani ya chumba cha habari,” alisisitiza.
Alisema
waandishi wa habari wanapaswa kuliheshimu hili, lakini pia viongozi wa vyumba
vya habari na wamiliki wa vyombo vya habari wanapaswa kulisisitiza na kulitolea
miongozo iliyo wazi ndani ya vyumba vya habari.
“Sisi tunavyoona ni kwamba, ikimpendeza mtu
kwenda kwenye siasa, aende kwenye siasa moja kwa moja, akitaka baada ya hapo
kujihusisha na kazi ya uandishi wa habari, ingependeza isiwe ndani ya chombo
cha habari, kwa sababu watu wataendelea kumtazama kama mgombea, kama kada,” alisema Kajubi.
Alifafanua
kuwa mwandishi wa habari ambaye amejihusisha na siasa za ushindani, anaweza
kuwa mwana safu (Columnist) lakini
chini ya safu yake ielezwe wazi kuwa huyu ni mwandishi wa siku nyingi na
aliwahi kugombea kupitia chama flani cha siasa.
"Hii
itasaidia hata mtu atakayeisoma safu yake au maoni yake aweze kujua mtu huyu
anatokea wapi, na ana msimamo gani, hilo ni jambo la muhimu ambalo kila chombo
cha habari ni lazima kikaweka utaratibu wake",alieleza.
Akizungumzia
kuhusu chombo cha habari kuwa na msimamo na chama fulani, alisema si dhambi
hata kidogo, na kuongeza kuwa katika historia ya vyombo vya habari hasa vya magazeti
wakati yanaanzishwa huko Ulaya, yalikuwa yanaanzishwa yakiwa ya kutetea hoja za
vyama vya siasa.
“Chombo
cha habari kinaanzishwa na kinajulikana kwamba hiki ni cha mlengo wa kushoto, au
cha sera za labour, hiki ni cha mlengo wa kulia, kinasimamia sera za conservative ndivyo vilivyoanzishwa,”alifafanua.
Aliwakumbusha
waandishi wa habari kuwa kazi ya uandishi wa habari inamtaka mwandishi wa
habari aonyeshe kwamba anaweza kutenda haki wakati wa uchaguzi kwa maana asipendelee
upande wowote, wala asiuminye upande mwingine kwa faida ya upande unaoupenda yeye.
Aidha
alivitaka vyombo vya habari vyenye lengo la kuonyesha mapenzi kwa chama fulani,
kuweka wazi lakini nia hiyo, bali visigeuke
kuwa vyombo vya propaganda kwa maana visiseme uongo, na badala yake viendelee
kutoa haki sawa, visikandamize upande mmoja na visinyime upande mwingine haki
ya kusikika, visiseme uongo, visipakazie upande mwingine kwa manufaa ya upande
wake na visichanganye maoni ndani ya habari
kwa manufaa ya chama chao.
Alisema
waandishi wa habari wajitahidi kubaki kuwa wanahabari, “Mimi ningependa hii
tasnia iwe na heshima, na iheshimiwe, ni kazi yenye majukumu makubwa, na
ningependa waandishi wa habari wazuri wajitahidi kubaki katika taaluma hii,”alisema
Bw. Kajubi.
Aliwaasa
waandishi wa habari kutenganisha mapenzi ya kisiasa, ushabiki, na uandishi wa
habari.
“Taaluma ibaki kuwa taaluma, na wanaotaka kwenda kwenye siasa,
hawakatazwi waende kwenye siasa, na wafanye hivyo mapema, na wafanye hivyo kila
mtu ajue, na wasiendelee kukaa ndani ya vyombo vya habari, au kukaa na vyeo vya
kusimamia waandishi wa habari wakati wao tayari ni makada walioingia katika
siasa za ushindani,” alisisitiza.
Social Plugin