Na Mwandishi Wetu- Dodoma
Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limetangaza majina ya vijana waliohitimu kidato cha sita kutoka shule zote za Tanzania Bara waliochagulwa kujiunga na mafunzo ya Jeshi hilo kwa mujibu wa sheria ya mwaka 2020 .
Akizungumza leo Julai 16, 2020 Makao Makuu ya Jeshi hilo Wilayani Chamwino Mkoani Dodoma, Mkuu wa Tawi la Utawala, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Kanali Julius Kadawi amesema kuwa Mkuu wa JKT Meja Jenerali Charles Mbuge anawakaribisha waliochaguliwa kujiunga na vijana wenzao katika kujifunza uzalendo, umoja wa kitaifa, stadi za kazi, stadi za maisha , utayari wa kulijenga na kulitumikia Taifa kupitia mafunzo hayo.
“Orodha kamili ya majina ya vijana waliochaguliwa, maeneo ya makambi ya JKT waliyopangiwa na vifaa wanavyotakiwa kwenda navyo inapatikana katika tovuti ya JKT ambayo ni www.jkt.go.tz”, Alisisitiza Kanali Kadawi.
Aidha, Kanali Kadawi amesema kuwa vijana hao wanatakiwa kuripoti makambini kuanzia tarehe 24 hadi 27 Julai, 2020 ambapo mafunzo yatafunguliwa rasmi Agosti 1, 2020.
Akifafanua, Kanali Kadawi amesema kuwa kwa upande wa wahitimu wenye ulemavu wa kuonekana kwa macho (Physical disabilities) wanatakiwa kuripoti katika kambi ya JKT Ruvu iliyopo Mlandizi mkoani Pwani ambayo ina miundombinu ya kuhudumia watu wa jamii hiyo.
“Kutokana na Ugonjwa wa Homa kali ya Mapafu (COVID -19) nchini, Tahadhari za kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo kama ilivyoelekezwa na Serikali kupitia Wizara ya Afya zitazingatiwa kwa kipindi chote vijana watakapokuwa katika mafunzo”, Alisisitiza Kanali Kadawi.
Vijana waliochaguliwa wamepangiwa katika kambi za JKT Rwamkoma- Mara, JKT Msange- Tabora, JKT Ruvu-Pwani, JKT Mpwapwa Dodoma, JKT Mafinga- Iringa, JKT Mlale-Ruvuma, JKT Mgambo na JKT Maramba- Tanga, JKT Makuyuni- Arusha, JKT Bulombora, JKT Kanembwa, JKT Mtabila- Kigoma, JKT Itaka- Songwe, JKT Luwa na JKT Milundikwa- Rukwa, JKT Nachingwea- Lindi,JKT Kibiti na Oljoro- Arusha.
Bofya Kuona Majina Hayo
Social Plugin