Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli
Rais John Magufuli ameelezwa kukerwa na kitendo cha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) kuomba fedha kiasi cha shilingi bilioni 1 za kujenga ofisi wilayani Chato mkoani Geita wakati tayari wana ofisi.
“Mmesema hapa mnataka kujenga ofisi ya TAKUKURU wilayani Chato, lakini tulishawapa jengo tena la ghorofa. Msizungumze mambo kwa kunifurahisha mimi, mjipendekeze Chato wakati nimeshaondoka kwenye Urais,” ameeleza Rais Magufuli.
Rais Magufuli amesema hayo katika hafla ya kuzindua majengo saba ya taasisi hiyo jijini Dodoma ambapo pia ameeleza kutoridhishwa na gharama zilizotumika kuyajenga kwa sababu ni kubwa sana.
Amesema kuwa tayari moyo wake umekuwa sugu hivyo hawezi kufurahishwa na mtu anayezungumzia Chato kwa sababu yeye si mbinafsi.
Akitilia mkazo katika hilo ameiagiza taasisi hiyo kumchunguza mtumishi aliyependekeza ijengwe ofisi nyingine Chato wakati tayari kuna ofisi na kwamba kitendo hicho kinaweza kuwa na dalili za rushwa.
Mbali na kuipongoza taasisi hiyo kwa kazi kubwa inayofanya kukabiliana na rushwa nchini, lakini amesema ina mapungufu ikiwa ni pamoja na kushindwa kuwachukulia hatua stahiki watumishi wake wanaotenda vitendo vya rushwa pamoja na kuchelewesha kupeleka kesi za rushwa mahakamani.
Akizungumzia gharama za nyumba hizo alizozizindua leo, amesema ni kubwa sana ikilinganishwa na hali halisi ya nyumba zenyewe, lakini ameamua kuzizindua kwa heshima kutokana na kazi kubwa ambayo TAKUKURU wamekuwa wakifanya.
Katika hatua nyingine ameahidi kutoa shilingi bilioni 2 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za watumishi wa TAKUKURU jijini Dodoma, na ameagiza Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) lipewe tenda ya kujenga nyumba hizo mara baada ya eneo la kujenga litakapopatikana.
Ameiasa taasisi hiyo kuendelea kukabiliana na vitendo vya rushwa hasa kipindi hiki cha uchaguzi mkuu ili kuhakikisha wananchi wanapata viongozi wanaowataka na sio wale wanaotwaa madaraka kwa kutumia nguvu ya fedha zao.