MAKAMU WA RAIS MGENI RASMI CRDB BANK MARATHON, SHILINGI MILIONI 200 KUKUSANYWA KUSAIDIA UPASUAJI WA MOYO KWA WATOTO 100

Dar es Salaam, Julai 21, 2020 – Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amemshukuru Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kuwa mgeni rasmi katika mbio za kwanza za hisani za “CRDB Bank Marathon” zinazolenga kuhamasisha uchangiaji wa shilingi milioni 200 kusaidia gharama za matibabu kwa watoto 100 wenye uhitaji wa upasuaji wa moyo. Nsekela ameeleza hayo katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika makao makuu ya Benki ya CRDB, Azikiwe Jijini Dar es Salaam.

Nsekela alisema mbali na makamu wa Rais, viongozi mbalimbali ikiwamo Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete pamoja na Waziri wa Michezo, Harisson Mwakyembe wanatarajiwa kuungana na maelfu ya wakimbiaji kushiriki CRDB Bank Marathon tarehe 16 Agosti, 2020 katika viwanja vya “The Greens” Oysterbay, Dar es Salaam.

“Kauli mbiu ya mbiu yetu katika mbio hizi za hisani ni ‘Kasi Isambazayo Tabasamu’, ikihamasisha watu wengi zaidi kujitokeza kushiriki kuleta tumaini la maisha na kusambaza tabasamu kwa Watoto wenye magonjwa ya moyo,” aliongezea Nsekela huku akibainisha kuwa CRDB Bank Marathon mwaka huu inategemea kuwa na washiriki zaidi ya 4,000.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (katikati) akizungumza katika mkutano na Waandishi wa habari wakati wa kutambulisha mbio za hisani “CRDB Bank Marathon 2020” zinazoandaliwa ili kuhamasisha uchangiaji wa fedha kwa ajili ya upasuaji kwa watoto wenye magonjwa ya moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete jijini Dar es salaam, leo. Nsekela alisema CRDB Bank Marathon inatarajiwa kukusanya shilingi milioni 200 ambapo washiriki zaidi ya 4,000 wanatarajiwa kushiriki siku hiyo tarehe 16 Agosti,2020 jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete, Prof. Mohamed Janabi na kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Sanlam Insurance, Khamisi Suleiman. 

Akizungumzia ushirikiano uliopo baina ya Benki ya CRDB na Taasisi ya Moyo katika kusaidia matibabu kwa watoto wenye matatizo ya moyo, Nsekela alisema kwa Benki ya CRDB imekuwa ikitoa msaada wa gharama za matibabu ambapo mwaka jana ilitoa shilingi milioni 100 kwa ajili ya upasuaji wa moyo kwa Watoto 50 na mapema mwaka huu ilitoa shilingi milioni 50 kwa ajili ya Watoto 25.

“Pamoja na jitihada za Serikali kupitia Taasisi ya Moyo kwa kushirikiana na wadau wengine ikiwamo Benki yetu ya CRDB bado watoto wengi wamekuwa wakikosa matibabu kutokana na wazazi au walezi kutomudu gharama za upasuaji ambazo ni kati ya Shilingi Milioni 2 hadi Milioni 20,” alisema Nsekela huku akibainisha kuwa CRDB Bank Marathon inatoa fursa kwa wadau mbalimbali ikiwamo watu binafsi na Taasisi kushiriki kuchangia matibabu.

Nsekela alizishukuru taasisi za Sanlam, Strategis, Alliance, ARIS, Cool Blue, EFM na TVE na wengineo kwa kujitokeza kushirikiana na Benki ya CRDB kufanikisha CRDB Bank Marathon, huku akihamasisha watu wengi zaidi kujitokeza kushiriki kwa kujisali kupitia tovuti maalum ya crdbtz.co/marathon.

“Kujisajili ni rahisi sana, unaweza kujisajili binafsi na kuchangia shilingi 30,000 au kupitia vikundi na kuchangia 25,000 kwa kila mmoja kupitia matawi ya Benki ya CRDB, CRDB Wakala, SimBanking App na mitandao ya simu (M-Pesa, TigoPesa, AirtelMoney). Fedha hizi zote zitaelekezwa katika kusaidia gharama za upasuaji wa watoto wenye magonjwa ya moyo,” alisema Nsekela.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete, Prof. Mohamed Janabi (kulia) akizungumza katika mkutano na Waandishi wa habari wakati wa kutambulisha mbio za hisani “CRDB Bank Marathon 2020” zinazoandaliwa ili kuhamasisha uchangiaji wa fedha kwa ajili ya upasuaji kwa watoto wenye magonjwa ya moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete jijini Dar es salaam, leo. 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Profesa Mohamed Janabi aliishukuru Benki ya CRDB kwa kuwa mstari wa mbele kusaidia jitihada za utoaji huduma za upasuaji moyo kwa Watoto. Profesa Janabi alitumia fursa hiyo pia kuwahamasisha Watanzania kujisajili kwa wingi kushiriki mbio hizo za hisani ili kusaidia upasuaji kwa watoto.

“Takwimu zinaonyesha watoto milioni 2 wanazaliwa nchini Tanzania wakati asilimia 1 kati yao huwa na magonjwa ya moyo. Ni wajibu wetu sisi kama jamii kuhakikisha watoto hawa wanapata matibabu stahiki, hivyo ushiriki wetu katika mbio hizi za hisani utusaidia kusambaza tabasamu kwa watoto hawa” alisema Profesa Janabi.
Akihitimisha mkutano huo Nsekela alisema Benki ya CRDB imejiwekea Sera maalum ya kusaidia jamii “Corporate Social Responsibility Policy” ambayo inaelekeza asilimia 1 ya faida ya kutumika katika kusaidia jamii katika sekta za elimu, afya na mazingira, ambapo mwaka jana pekee Benki ilitoa zaidi ya shilingi bilioni 1.2.

“Uanzishwaji wa mbio za hisani za CRDB Bank Marathon utasaidia kuongeza ushiriki wa wadau wengi zaidi katika Maendeleo katika sekta hizi za afya, elimu na mazingira,” alisema Nsekela.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post