MGEJA : SIONI CHAMA CHA KUISHINDA CCM 2020

Khamis Mgeja
Na Paul Kayanda - Kahama 
MWENYEKITI wa taasisi ya Tanzania Mzalendo Foundation Khamis Mgeja amesema kuwa wakati Taifa likielekea katika uchaguzi mkuu 2020 ili kuwapata viongozi ngazi ya Urais Ubunge na Udiwani haoni chama cha kukishinda Chama cha Mapinduzi (CCM).


Mgeja aliyasema hayo jana alipokuwa akiongea na Waandishi wa Habari waliomtembelea nyumbani kwake katika kijijini cha  Nyanhembe Kata ya Kilago Halmashauri ya Mji wa Kahama Mkoani Shinyanga kwa ili kupata maoni yake binafsi na mtazamo wake kuhusu mustakabali wa nchi kuelekea uchaguzi mkuu wa 2020.

Mwenyekiti huyo wa taasisi ya Mzalendo Foundation inayojishughulisha na masuala ya demokrasia haki na utawala bora alisema kuwa mtazamo wake na uzoefu mkubwa wa masuala ya siasa na mahusiano ya jamii haoni chama chochote hivi sasa nchini cha kushindana na kukishinda chama cha Mapinduzi CCM.

Mgeja alisema kuwa zipo sababu nyingi za kusababisha CCM kishinde kwa kishindo na kupelekea vyama vya upinzani kuanguka kwa kishindo.

Aliendelea kuwaeleza waandishi wa habari kuwa sababu kubwa moja ni kupitia serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Joseph Pombe Magufuli ni utekelezaji wa kiwango cha hali ya juu sana kuhusu utekelezaji wa ilani ya chama cha Mapinduzi katika Nyanja zote za huduma ya jamii.

Alisema kuwa pia ni uzalendo wa mheshimiwa Rais Magufuli alioufanya katika Taifa na kuongeza kuwa tatu ni uadilifu wake kuhusu kuisimamia serikali anayoiongoza kwa uadilifu wa hali ya juu sana.

Mgeja alisema kuwa sifa nyingine ni Rais kuwa mjasili na kuthubutu kuyatekeleza mambo makubwa hususani miradi iliyokuwa imeshindikana kutekelezwa katika miaka ya nyuma ikiwamo mradi mkubwa wa uzalishaji umeme katika Mto Rufiji, reli ya kati, serikali kuhamia Dodoma pamoja na mambo mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi.

Mgeja alisema kuwa kwa sababu hizo za utekelezaji wa miradi mbalimbali ndiyo sababu pekee itakayopelekea CCM kushinda kwa kishindo kikubwa sana na kupelekea kwa mafanikio hayo makubwa yanayomwekea Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli njia nyeupe ya kwenda Ikulu oktoba 2020.

Akizungumzia kuhusu upinzani alisema kuwa sababu kubwa zitakazopelekea kushindwa kwa kishindo kwa mwaka huu wa 2020 kwa vyama vyote vya upinzani sababu moja wapo ni wanaingia mwaka huu wakiwa hawana agenda yoyote ile inayogusa nchi na maisha ya watu badala yake yote yanatekelzwa na CCM.

Alisema kuwa katika kpindi cha miaka mitano iliyopita kutokea uchaguzi wa mwaka 2015 wamekosa sela nzuri mbadala dhidi ya chama tawala CCM sela ambayo wangekuwanazo wangewajengea imani wananchi na kujijenga wao.

Tatu vyama vya upinzani kukosa utayari wa kuongoza nchi ikiwemo mfano mkubwa katika tatizo hili la kukabiliana na Gonjwa la Corona COVID-19 huku akitolea mfano wa chama kikuu cha upinzani kikikimbia bungeni na kuhoji kuwa je? Kama taifa likipata misukosuko ya njaa au vita itakuwaje ikiwa na viongozi ambao hawana utayari na ujasiri.

 “Nne sioni kiongozi hivi sasa wanaosemwa semwa kutokea upinzani wenye sifa au vigezo vinavyokidhi uwezo wa kuwa Rais ili kuiongoza nchi, alisema Mgeja mwenyekiti wa taasisi ya Mzalendo Foundation.

Mgeja alisema kuwa wapinzani wakikosa sifa zote hizo maana yake wataingia katika kinyan’ganyilo cha uchaguzi mwaka huu 2020 wakiwa wamefirisika ni vyema kama vyama makini wakajitathmini.

Pia alivishauri kwa vyama vyote vya upinzani wawe wastaarabu na kukubali matokeo mapema ya kushindwa watakuwa wamejijengea heshima kubwa sana kwani si busara wakashiriki uchaguzi huku wakijua wanaenda kushindwa ni sawa na Simba, Yanga, Azam zinaingia fainali na kucheza timu za mchangani unategemea nini katika matokeo ya ubingwa.

“Pamoja na kuwa wote tunapenda na kuheshimu demokrasia lakini demokrasia inayokosa ushindani hayo ni matumizi mabaya ya demokrasia na raslimali za nchi kwani mabilioni ya fedha yatakayotumika na kuteketea bure hiizo ni kodi za wananchi na hasa wanyonge ingekuwa vyema fedha hizo kujielekeza kwenyenye huduma za jamii ikiwemo afya, elimu, barabara, umeme na miundombinu mingine ikiwemo reli,” alisema Mgeja.

Alisema kuwa japo ukweli unauma lakini ukweli utabaki palepale na kunausemi wa waswahili unaosema, heri aibu kuliko fedheha na kuwashauri wapinzani wakubali yaishe kwani katika siasa kuna wakati mnaweza kutofautiana na wakati mwingine mnaweza kukubaliana katika masuala ya msingi yanayohusu mstakabali wa Taifa.

“Ni busara na kukomaa kisiasa kukubali na kupongeza unapoona mshindani wako anapofanya vizuri  na kumuunga mkono aendelee kuongoza nchi kama TLP walivyounga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano binafsi nawapongeza TLP kupitia mwenyekiti wao mheshimiwa Augustino Lyatonga Mrema kwa kuonyesha uungwana wa kisiasa nawaomba wanasiasa na vyama vingine viige mfano huo ili tuungane pamoja katika kuleta maendeleo kwa wananchi,” alisema Khamis Mgeja.

Mgeja ambaye ni mwanasiasa mkongwe nchini ambaye ameamua kupumzika siasa na kujikita kijijini na kujishughulisha na suala la kilimo na ufugaji.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post