Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MKANDARASI WA MAJI IRINGA APEWA WIKI NNE KUKAMILISHA MRADI


NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga ametoa Wiki Nne kwa Mkandarasi Kampuni ya GNMS Contractors ya Iringa na Kampuni ya Hematec Investiment ya Dar es Salaam kukamilisha ujenzi wa mradi wa maji wa Pawaga- Mlenge, Wilayani Iringa.

Mhandisi Sanga ametoa maelekezo hayo Julai 16, 2020 alipofanya ziara kwenye mradi huo ili kujionea hatua ya utekelezwaji wake sambamba na kuzungumza na wakandarasi wanaoutekeleza ambapo alielezwa kuwa mradi utaanza kutoa maji baada ya miezi miwili ijayo.

Mhandisi Sanga hakuridhishwa na kasi ya utekelezwaji wa mradi na hakukubaliana na maelezo ya kukamilisha mradi baada ya miezi miwili hasa ikizingatiwa kwamba lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwanza kabla ya kukamilisha shughuli zingine za mradi.

“Serikali ilikwishaelekeza miradi yote ya maji inapasa kwanza itoe maji ili wananchi waanze kunufaika na sio kusubiri hadi ujenzi wa matenki ukamilike ndipo wananchi wapate huduma wakati inawezekana kabisa wakapata maji kabla hayajafika kwenye haya matenki mnayojenga,” alisisitiza Mhandisi Sanga.

Alisema miradi haipaswi kuchelewa bila kuwa na sababu ya msingi na alibainisha kwamba malipo kwa wakandarasi yamekuwa yakifanyika kwa wakati lakini hayaakisi hali halisi ya kasi ya utekelezaji inayodhamiriwa na Serikali.

Mhandisi Sanga alisema Pawaga ni eneo lenye ukame na kwamba wananchi wanapata tabu kukosa huduma ya maji na wakati huohuo wakandarasi wanalipwa kwa wakati lakini kasi yao sio ya kuridhisha.

Alielekeza Mamlaka ya Maji Iringa (IRUWASA) na Wakala ya Maji Vijijini (RUWASA) kushirikiana kusimamia utekelezaji wa miradi.

“Hatuwezi kutoka Dodoma kuja huku kusisitiza wakandarasi waongeze kasi wakati nyie huku ni wasimamizi wa miradi kwa niaba ya Wizara, hakikisheni miradi mnayoisimamia inakamilika kwa wakati na kipaumbele ni wananchi kwanza kupata maji,” alisisitiza Mhandisi Sanga.

Aidha, Mhandisi Sanga aliwakumbusha wasimamizi wa miradi kote nchini kuhakikisha kwenye utekelezaji wa miradi wanaanza na maeneo yatakayoleta matokeo ya haraka ili wananchi waanze kupata huduma na baadaye waendelee na maeneo mengine wakati ambao tayari wananchi wanakuwa na huduma.

“Mnatakiwa kuwa wabunifu wakati wa ujenzi wa miradi, mnapaswa kuanza na maeneo yatakayoleta matokeo ya haraka ili kwanza wananchi wapate huduma na huku mkiendelea kutekeleza maeneo mengine,” alisisitiza Mhandisi Sanga.

Kwa upande wake Meneja Ufundi wa IRUWASA, Mhandisi Fabian Maganga akizungumzia utekelezawaji wa mradi, alisema unatekelezwa kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP) na Programu ndogo ya maji na usafi wa mazingira vijijini (RWSSP) kwa gharama ya Shilingi Bilioni 5.2.

Mhandisi Maganga alisema mradi umelenga kuwaondoshea kero ya maji wananchi wa Kata za Ilolompya, Mboliboli, Itunundu na Mlenge waliopo katika vijiji 14 na kwamba utanufaisha wakazi wapatao 30,258.

Mara baada ya kamilisha ziara yake kwenye mradi wa Pawaga-Mlenge, Naibu Katibu Mkuu, Mhandisi Sanga alihitimisha ziara yake kwenye mradi wa Tenki la Ilula la lita 500,000 ambalo linahudumia zaidi ya wakazi 35,000 kutoka Kata za Nyalumbu na Ilula ambapo alisisitiza kutazama namna ya kupanua utoaji wa huduma kwa maeneo mengine ya jirani.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com